Makete.
Wananchi wilayani Makete wameshauriwa kutumia ipasavyo huduma zinazotolewa na vituo vya matunzo na tiba (CTC) ambazo zinazidi kusogezwa karibu nao kila kukicha wilayani humo, ili kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi na kupelekea nguvu kazi ya Wilaya hiyo kuzidi kupungua
Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkuu wa wilaya ya makete Mh. Zainabu Kwikwega katika risala ya ufunguzi wa kituo cha CTC katika kijiji cha Mang’oto wilayani humo iliyosomwa kwa niaba yake na Mganga mkuu Wilaya ya Makete Dk. Joseph Gasper.
Alisema Kituo hicho ni cha tatu kufunguliwa na kuanza kutoa huduma tangu Oktoba waka jana hadi Januari mwaka huu kwa ufadhili wa shirika lisilokuwa la kiserikali la CUAMM kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Makete na kukamilisha idadi ya kliniki za matunzo na tiba zilizopewa namba za usajili kufikia 11
“Kusema kweli hatuwezi kuacha kuwashukuru wafadhili wetu ambao ni shirika la CUAMM kwani wamechangia kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa kituo hiki na si hiki tuu kwani wametusaidia katika kituo cha CTC Ujuni na kile cha Lupalilo hivyo tunashukuru sana ” ilisema sehemu ya risala hiyo.
Aliwataka kuhakikisha wale wote wanaopata huduma za CTC katika hospitali ya wilaya Consolata Ikonda kwenda katika hospitali hiyo na kutoa taarifa ya kuomba kuhama ili wapate huduma katika kituo hicho kilichofunguliwa ambacho kipo katika kijiji chao.
Baada ya kutoa taarifa hizo watapatiwa fomu maalum watakazozijaza na kuzipeleka katika kituo hicho ambacho watahamia kwa ajili ya kuanza kupatiwa huduma hizo ambapo kwa kufanya hivyo watakuwa wamesajiliwa kupata huduma hapo hivyo haina haja ya kwenda katika kile kituo cha awali.
“Serikali imeona mateso mliyokuwa mkiyapata wakati mkitembea umbali wa zaidi ya kilomita 12 kwa miguu kufuata huduma za CTC kule Consolata Ikonda, lakini tumshukuru Mungu kuwa serikali imeliona hilo , kazi kwenu kuhakikisha mnatumia ipasavyo huduma hii”
Kabla ya kusoma risala hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Mganga mkuu Dk. Joseph Gasper amewataka wakazi hao wa Mang’oto na vijiji vya jirani kuhakikisha wanajiunga na Mfuko wa matibabu wa CHF ambao utawawezesha wanachama wake kulipa ada ya shilingi 5000 kwa mwaka ili wapatiwe matibabu bure kila waendapo hospitalini kwa mwaka
Baada ya mwanachama kulipa ada hiyo ya shilingi 5000 itawezesha yeye na familia yake (Jumla wawe watu sita) kupata matibabu katika hospitali bila kuulizwa fedha yeyote hadi mwaka uishe ndipo alipe tena 5000 nyingine
“Nitoe mfano endapo una familia yenye watoto sita halafu kwa bahati mbaya mkala chakula kikawaletea madhara ya tumbo mkienda hospitali kila mmoja atalipa shilingi 1000 ambapo kwa ninyi nyote mtalipa shilingi 6000 gharama ambayo ni kubwa kuliko ada ya CHF kwa mwaka ambapo kama mngekuwa mmejiunga na mfuko huo mngetibiwa bure” alisisitiza Dk. Gasper.
Pia Dk. Gasper aliwashauri kutumia huduma hiyo ya CTC katika kituo hicho ila ambaye ana uwezo wa kuendelea na kituo cha Hospitali ya Consolata Ikonda ni ruksa kufanya hivyo kwani ni hiari yao kwenda kupata huduma za CTC katika kituo chochote anachokipenda.
Kwa upande wake Mratibu wa Ukimwi wilaya ya Makete (DAC) Bw. Shadrack Sanga alisema “huko nyuma watu walikuwa wakipoteza maisha kwa UKIMWI tofauti na ilivyo sasa kwani zipo dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi ARV’s na watu wanazitumia ila bado idadi ni ndogo hivyo tusione aibu kuzitumia”
Naye mratibu wa shughuli za Ukimwi katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete (CHAC) Bi. Ester Lamosai aliwataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi kupima virusi vya Ukimwi kwa hiari kwani itawezesha kupatikana kwa takwimu sahihi za maambukizi mapya ya VVU katika Wilaya ya Makete
Aliongeza kuwa watu wakifahamu hali ya afya zao ni rahisi kujichunga na kutoeneza VVU kwa makusudi kwa wale watakaokutwa wana maambukizi na wale wasio na maambukizi watajichunga zaidi
“Mtu ukijua hali yako ya afya unapunguza madhara mengi ikiwemo wale walio na VVU kutoambukiza kwa makusudi wale wasio na VVU na pia kama vitabu vya dini vinavyosema kuwa kila mtu atahukumiwa kulingana na aliyoyafanya jamani tuepuke adhabu hii kwa kuogopa kuwaambukiza watu wasio na hatia” alisema Lamosai
Hadi Desemba 2010 watu waliopima na kugundulika kuwa na maambukizi ya VVU ni 10,002 ambapo kati yao wanaume ni 3963 na wanawake ni 6039 na miongoni mwao walioanzishiwa dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI(ARV’s) ni 3632, wanawake wakiwa 2124 na wanaume ni 1508.
Mwisho