HIZI FEDHA ZITUMUKE IPASAVYO

Makete

Mkuu wa wilaya ya Makete Zainab Ahmad Kwikwega

Hundi zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5 zimetolewa na Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Zainab Ahmad Kwikwega ikiwa ni ahadi alizozitoa kwa shule mbalimbali za sekondari wilayani Makete wakati wa ziara yake katika shule hizo Desemba 20-22 mwaka jana

Akiongea na Kwanza Jamii ofisini kwake Mh. Kwikwega alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu wilayani humo hasa kuboresha mandhari ya shule husika hususan kwa kidato cha kwanza walioanza masomo yao januari 10, 2011.

“Unajua Mungu kanijalia mwishoni mwa mwaka jana nilifanikiwa kufanya ziara katika shule zote za kata zilizopo hapa wilayani, na wewe mwandishi ni shahidi kuwa tulikuta zina changamoto nyingi hivyo kwa kuwa ninapenda elimu ndio maana nimetoa fedha hizo” alisema Mh. Kwikwega

Akifafanua kuhusu hundi hizo Mkuu huyo amesema Shule ya Sekondari Ukwama imepata hundi ya sh. Milioni 1.5, ambazo ni kwa ajili ya kuendeleza kujenga darasa moja ambalo lilikuwa katika hatua ya paa pamoja na kusaidia kujenga chumba kingine cha darasa ambacho kilikuwa katika hatua ya msingi.

Lupila sekondari imepata hundi ya shilingi Milioni 1 ambazo amesema ni kwa ajili ya ukarabati wa sakafu katika baadhi ya vyumba vya madarasa pamoja na kupaka rangi kwenye vyumba vya madarasa ya kidato cha kwanza kwani shule hiyo ni miongoni mwa shule kongwe zilizopo wilayani Makete hivyo inahitaji ukarabati.

Nayo shule ya sekondari Kipagalo imepewa hundi ya  shilingi 500,000 kwa ajili ya kufanya ukarabati mdogo wa vyumba vya madarasa shuleni hapo huku Kitulo sekondari ikipatiwa hundi ya shilingi 200,000, Matamba sekondari wakipata shilingi 300,000 na Usililo wakipata hundi ya shilingi 500,000 kwa ajili hiyo hiyo

Shule ya sekondari Mwakavuta imepata hundi ya shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa bwalo na jiko kwani shule hiyo yenye kidato cha tano walioanza masomo mwaka jana ni aibu kukosa bwalo ingawa ina jiko lakini halikidhi uwezo unaohitajika

Katika hatua nyingine Kijiji Cha Ikovo kilipatiwa hundi ya shilingi 81,000 kwa ajili ya kununulia saruji kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa ofisi za serikali ya kijiji hicho ambacho wakazi wake walihamishiwa hapo kutoka katika kijiji cha Ikovo ya zamani ambacho kwa sasa ni hifadhi ya Taifa.

“Ninapongeza sana jitihada za wakazi wa kijiji cha Ikovo kwa kujitoa kujenga ofisi za kisasa za kijiji chao, kwani imebaki umaliziaji mdogo tu hasa unaohitaji saruji, hivyo fedha hizo zitawasaidia katika umaliziaji huo” alisema Kwikwega

Alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kufanyia shughuli za kimaendeleo katika kila shule na kijiji hicho kuligana na changamoto zilizojitokeza wakati akifanya ziara katika shule hizo kwani atahakikisha anafuatilia ipasavvyo mwenendo mzima wa matumizi ya fedha hizo.

“Natoa onyo kali kwa kiongozi yeyote ambaye amepewa fedha hizo halafu akazitumia tofauti na makubaliano yaliyopo kwani nitafuatilia hatua baada ya hatua bila kuwapa taarifa, yeyote nitakayekuta ametumia fedha hizo ndivyo sivyo nitamchukulia hatua kali za kisheria” alisisitiza.

Desema 20 – 22 mwaka jana Mh. Kwikwega alifanya ziara katika shule zote za sekondari za kata wilayani Makete ili kuangalia maandalizi waliyofanya ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochaguliwa kujiunga na shule hizo ambazo ni Kipagalo, Matamba, Mlondwe, Iwawa, Mwakavuta, Mountain Chafukwe, Usililo, Mang’oto, Ipelele, Ikuwo, Lupalilo, Ipepo, Lupila, Ukwama, Kitulo na Mbalache ambapo jumla ya wanafunzi 2012 walifaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule hizo.

Mwisho

Na Edwin Moshi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo