Serikali yasitisha usajili wa taasisi ya dini

 


Wizara ya Mambo ya Ndani imesitisha usajili wa Jumuiya ya kidini iitwayo Spirit Word Ministry iliyopo eneo la Stakishari Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam baada ya kubainika kutoa mahubiri na mafundisho yenye mwelekeo wa kuhamasisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.


Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni ameyasema hayo leo Jumatatu wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2023/24.

Masauni amesema katika kudhibiti na kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili Ofisi ya Msajili wa Jumuiya imesitisha shughuli za Jumuiya ya kidini iitwayo Spirit Word Ministry iliyopo eneo la Stakishari Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

“Jumuiya hiyo imefutiwa usajili kwa sababu ya kutoa mahubiri na mafundisho yenye mwelekeo wa kuhamasisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na kutoa ujumbe wenye kuhafifisha jitihada za kupambana na vitendo vya ushoga nchini,”amesema.

Aidha, Masauni amesema taarifa zimekusanywa zinazohusu idadi ya vituo vya kulea watoto na shule zinazotoa mafundisho ya dini kwa watoto wadogo.

Amesema lengo ni kutambua idadi ya vituo au shule za bweni zinazotoa mafunzo yenye mwelekeo unaokinzana na maadili ya nchi yetu ikiwemo vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.

Amesema katika mwaka 2023/24 wizara imepanga kuandaa mwongozo wa taratibu za kuabudu na ithibati ya taasisi zinazotoa elimu ya dini, kuimarisha ufuatiliaji na utendaji wa Jumuiya za Kidini na zisizokuwa za Kidini.

Pia amesema katika mwaka huo watafanya ukaguzi na tathmini ya vihatarishi vya kiusalama kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na kutoa mafunzo kwa Viongozi wa Jumuiya yatakayochangia kudumisha amani na utulivu nchini.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo