Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limetoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa mitandaoni kumhusu Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini na Mmiliki wa Kiwanda cha kuchakata Pamba kitwacho Mwalujo Ginery kilichopo Kijiji cha Mwalujo, Wilaya ya Kwimba, Hamisi Kingwangala kudaiwa kumpiga risasi Mlinzi wake Jumanne Omary Misango (66) katika mguu wa kulia, ambapo imebainika Jumanne hakupigwa risasi bali haliwaongopea Polisi.
RPC wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema taarifa za awali zinaonesha kulitokea wizi wa mali kiwandani ikiwemo Gear Motor HP Radio made 02, Electrical Motor 05 na nyaya za umeme Armored Cable Mita 25 vyote vikiwa na thamani ya Tsh 28,525,000.
"Mei 22, 2023 saa 11:00 jioni Kigwangala alifika kiwandani kwake na kukatokea majibizano kati yake na Mlinzi wake, Mlinzi huyo alitoa taarifa Polisi kuwa alishambuliwa na kupigwa risasi mguu wa kulia. Askari walifika eneo la tukio na kufanya ukaguzi ambapo hakukuonekena viashiria vyovyote vya matumizi ya silaha ya moto.
"Hata hivyo Jumanne alipewa PF3 na kwenda Hospitali ya Wilaya ya kwimba kwa uchunguzi wa kitabibuų, Hamisi Kigwangala alihojiwa na kufunguliwa kesi ya shambulio na yupo nje kwa dhamana.
"Uchunguzi umebaini kuwa hakuna jeraha wala mvunjiko wowote wa mfupa katika mwili wa Jumanne na hivyo amefunguliwa jalada la uchunguzi kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa Afisa wa Polisi na kuzua taharuki kwa Jamii kuwa amepigwa risasi.
"Upelelezi wa kesi hizo mbili unaendelea na utakapo kamilika Watuhumiwa wote wawili watafikishwa Mahakamani, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa Wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi."