Wavamia Kituo cha Polisi na Kutoweka na Mali ya Thamani ya milioni 4.3



Mauaji ya mwakilishi wadi wa Kisa Mashariki Stephen Maloba yameonekana kuwapandisha mori wakazi waliovamia kituo cha polisi cha Emasasi ambapo walitoroka na magunia 1,240 ya mbolea ya ruzuku yenye thamani ya shilingi milioni 4.3.


Mbolea iliyoibwa ilikuwa imetangwa kwa minajili ya kusambazwa kwa wakulima katika mpango wa serikali wa kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea yenye bei nafuu wakati huu wa upanzi. 


Pikipiki inayomilikiwa na chifu wa eneo hilo Walter Obushere iliteketezwa na kundi la vijana hao waliokuwa wakiandamana kulalamikia mauaji ya Maloba. 


Akizungumza na wanahabari baada ya kisa hicho chifu wa eneo hilo Obushere alionyesha kusikitishwa kwakwe na tukio hilo na kusema kuwa vijana walioharibu mali yake na kurusha mawe katika boma lake walikuwa wanafunzi.


“Vijana waliovamia boma langu walikuwa wadogo sana wengine walikuwa wanafunzi wa sekondari na wengine ni vijana wa shule za msingi. Sina ugomvi na mwakilishi wadi aliyefariki kwani alikuwa kaka yangu na tulifanya naye kazi vizuri. Kazi yetu kama machifu ni kufanya kazi na wale ambao wamechaguliwa,” Obushere alisema. 


Maafisa wa usalama wamesema kuwa walikuwa wamepata magunia 20 ya mbolea iliyoibiwa na kusema kuwa uchunguzi unandelea kubaini waliohusika katika tukio hilo. 


Mwakilishi wadi Stephen Maloba alifariki Aprili 1 baada ya kudungwa kisu katika purukushani inayokisiwa kuwa ya kisiasa iliyohusisha makundi mawili hasimu. Kifo cha Maloba kilitangazwa na Naibu Gavana Ayub Savula katika ibada ya maombi iliyoyaleta madhehebu 40 pamoja katika kaunti ya Kakamega. 

Chanzo: TUKO.co.ke 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo