Afia kwenye basi akienda kufuata maombi kwa Mchungaji


Mwanamke aliyefunga safari kutoka 
Bungoma kuelekea Mombasa huko nchini Kenya kutafuta maombi, alifariki dunia akiwa ndani ya basi.


Kwa mujibu wa ripoti ya polisi ya kituo cha Polisi cha Central, dereva wa basi la Simba Coach, Musa Moi Owalo alipiga ripoti kuwa Consolota Wesonga Otieno alikuwa akisafiri kutoka Bungoma kuelekea Mombasa alipofariki njiani.


Polisi walitembelea eneo la tukio na kupata maiti ya mwanamke huyo.

Baada ya kupekua mkoba wake, polisi walipata hati kadhaa za matibabu zilizoonyesha kuwa mwanamke huyo alikuwa akiugua maradhi yasiyojulikana.

"Mmoja wa abiria ambaye alikuwa akisafiri ndani ya basi alifariki njiani. Nilipofika niliwaarifu maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ambao walitembelea eneo la tukio na kupata maiti ya mwanamke huyo."

"Baada ya kupekua mkoba wake, hati kadhaa za matibabu zilipatikana ambazo zilifichua kwamba mwanamke huyo alikuwa akiugua maradhi yasiyojulikana," ripoti ya polisi ilisoma.

Kulingana na bintiye Faith Otieno, mama yake aliondoka Bungoma kuelekea Kilifi kutafuta maombi kwani amekuwa akiugua kwa muda mrefu.

Binti huyo alieleza kuwa mama yake alitakiwa kusafiri hadi Mombasa, na baadaye kwenda Kilifi kutafuta maombi kutoka kwa mchungaji maarufu ambaye aliamini atamponya.

Alifichua kwamba inasikitisha mama yake aliacha kutumia dawa zake na kuanza kumfuata pasta huyo maarufu ambaye hupeperusha ibada zake kwenye televisheni.

"Inasikitisha kwamba alifariki hata kabla ya kuonana na mchungaji huyo. Sasa ametuachia gharama za kusafirisha mwili wake na kulipia gharama za chumba cha maiti," binti huyo alilalamika.

Faith alisema waliarifiwa kuhusu kifo chake na polisi na sasa wanajianda kusafiri hadi Mombasa kushuhudia zoezi la uchunguzi wa maiti.

Mwili wa mwanamke huyo umehamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Coast General, ukisubiri kufanyiwa upasuaji.

Chanzo: TUKO.co.ke


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo