Wananchi wa kata ya Kifanya Halmashauri ya mji wa Njombe wanadaiwa kuficha taarifa za vifo vya wapendwa wao wanapofariki nyakati za jioni au usiku ili kuepuka gharama za kusafirisha miili zaidi Kilomita 50 mpaka Mochwari iliyopo hospitali ya mji wa Njombe Kibena.
Hayo yamebainishwa kwenye mdahalo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za mradi wa ufuatiliaji wa mapato na matumizi ya jamii kwenye sekta ya afya (PETS) unaofadhiliwa na shirika la Foundation For Civil Society unaotekelezwa na shirika la Highland Hope Umbrella (HHU) katika kata ya Kifanya.
Shigela Ganja ni mchumi wa Halmashauri ya mji wa Njombe, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri katika mdahalo huo amekiri uwepo wa changamoto ya Mochwari katika kata ya Kifanya huku akibainisha kuwa Halmashauri inajenga vituo vingi vya afya kwa mapato ya ndani hivyo wanaamini kushughulikia changamoto hiyo.
Katika maazimio ya mdahalo huo baadhi ya wajumbe wakiwemo wenyeviti vijiji kutoka kata hiyo licha ya mapendekezo mengine wameomba kujengwa Mochwari katika kituo cha afya Kifanya ili kuondoa adha wanayokutana nayo wananchi.