Mhasibu aliyetekwa na kuchomwa moto azikwa, baba afunguka ya moyoni

Hatimaye aliyewahikuwa mfanyakazi wa Benki ya BOA, Tawi la Kahama, Neema (Martha) Towo (30) amezikwa leo Jumatatu nyumbani kwao katika Kijiji cha Mrimbo, Mwika, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.


Inadaiwa kwamba Neema alitekwa na kuuawa kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana Machi 8 mwaka huu.

Taarifa za awali kutoka kwa baba yake, Ndeonasia Towo alieleza kuwa siku ya tukio Neema alikuwa kanisani kwenye ibada ya jioni, alipigiwa simu na watu asiowajua akiwa ndani ya kanisa, akatoka nje kusikiliza baada ya hapo hakuonekana tena.

Akitoa mahubiri wakati wa ibada ya mazishi katika Kanisa la KKKT, Usharika Uuwo, Mwika wilaya ya Moshi, Mwinjilisti John Ngowi amesema mauaji hayo hayapaswi kuvumilika na kwamba hakuna mwenye haki ya kuondoa uhai wa mwenzake.

Amesema maisha ya Neema yamekatishwa kikatili na kwamba ni jambo ambalo halikubaliki katika jamii yoyote ile kwani Mungu ndiye anayejua mwisho wa maisha ya mtu pekee.

"Maisha ya Neema yamekatishwa kikatili, hili halikubalika katika jamii yoyote ile kwani Mungu anataka watu wote waishi mpaka hapo Mungu alipoweka kikomo cha mtu kuishi hapa duniani," amesema.

Amesema kitendo hicho ni chukizo mbele ya Mungu na kwamba yupo Mungu mtetezi asimamaye akiwatetea wale waliodhulumiwa uhai wao.

Hata hivyo baba wa Neema, Ndeonasia Towo amewaomba waumini wa kanisa hilo kwa kuwa anayo kazi kubwa ya kwenda kufuatilia haki za mwanaye huyo ambaye ameuawa kikatili.

"Mniombee kwa sababu nitalazimika kwenda kufuatilia haki za mwanangu pamoja na mambo mengine, mniombee," amesema.

Chanzo:Mwananchi Digital


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo