Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyoketi Wilayani Mufindi imemhukumu kifungo cha miaka mitano(5) jela Wilbert Mpyagisa mwenye umri wa miaka 41 mkazi wa Kijiji cha Mkangwe Wilayani Mufindi kwa kosa la kumuua baba yake mkwe Mradi Kinyaga bila kukusudia.
Wilbert Mpyagisa alitenda kosa hilo aprili 10,2015 majira ya asubuhi huko kijijini kwao Mkangwe akimtuhumu baba yake mkwe kwamba ni mchawi akidai kuwa baba yake mkwe alimuua mtoto wake mwaka 2014 kwa ushirikina.
Baada ya kufikishwa Mahakamani mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo la kuua bila kukusudia chini ya kifungu namba 195 na 198 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 rejeo la mwaka 2002 ambapo mahakama ilimkuta na hatia mshtakiwa huyo.
Shauri hilo la mauaji namba 30 la mwaka 2016 limesimamiwa na Wakili wa Serikali Yahaya Misango ambapo aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa mtuhumiwa na kwa watu wengine wenye imani za kishirikina kama hizo kwa sababu tuhuma kama hizo zimeondoa watu wengi katika Taifa hili.
Kwa upande wa utetezi wa mtuhumiwa ukiongozwa na Wakili Msomi Vedasto Chonya aliiomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa sababu alikiri kosa na kuipunguzia gharama jamhuri kusikiliza shauri hilo na pia mteja wake ametenda kosa hilo kwa mara ya kwanza huku akibainisha kuwa mteja wake amekaa gerezani kwa muda wa miaka nane amejifunza na anajutia kutenda kosa hilo.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyoketi Mufindi Ilvin Mgeta amesema kwa kuzingatia pande zote mbili upande wa mashtaka na upande wa utetezi mahakama imetoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine.