Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Rumuruti nchini Kenya, ameuawa na wagemaji wa pombe za kienyeji maarufu kama chang'aa baada ya kumdunga kisu alipofika katika eneo wanalopikia pombe hizo.
Afisa huyo alidungwa kisu jana Alhamisi, Februari 16, 2023 alipofika katika eneo hilo akiwa kwenye bodaboda bila kujihami na silaha yoyote na kuanza kukabiliana na wagemaji hao.
Kamanda wa Polisi Kaunti ya Laikipia John Nyoike alisema kisa hicho kilitokea majira ya saa 2 usiku katika eneo la Maundu ni Meri.
"Imeripotiwa kuwa afisa huyo alipata taarifa kwamba kuna mitungi ya pombe iliyokuwa imeletwa eneo hilo, ndipo aliamua kuvamia eneo hilo," mkuu huyo wa polisi alisema.
"Mwendesha bodaboda ndiye alifika kuripoti kuwa mteja aliyepeleka eneo hilo alidungwa kisu baada ya ugomvi mkubwa kuibuka baina yake na mgemaji mmoja," ripoti hiyo iliongeza.