Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza mkuu wa mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na kamanda wa polisi wa mkoa huo wahakikishe wanamfikisha katika vyombo vya sheria baba mzazi wa mwanafunzi wa darasa la pili katika Kata ya Sokoni One anayetuhumiwa kumdhalilisha mtoto wake.
Akitoa agizo hilo Waziri Mkuu amesema serikali inakemea vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji kwa watoto, hivyo wakuu wote wa mikoa na makamanda wa polisi wa mikoa yote nchini wahakikishe wanawasaka na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo viovu.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kusambaa kwa taarifa kupitia vyombo vya habari vikimuonesha mtoto huyo anayedaiwa kudhalilishwa na baba yake mzazi.
Katika taarifa yake mtoto huyo amesikika akielezea namna mzazi wake huyo alivyokuwa akimfanyia vitendo vya ukatili.
Waziri Mkuu Majaliwa ametaka mtoto huyo naye atafutwe na kupatiwa huduma ya matibabu kwa haraka.
Amesisitiza kuwa serikali haitofumbia macho wala kukubaliana na vitendo vya ukatili kwa watoto, na hivyo ameitaka jamii kushirikiana katika kupiga vita vitendo hivyo pamoja na kutowaficha wale wote wanaohusika na unyanyasaji huo.