Wanafunzi wafukuzwa shule kwa kutolipa mchango wa mpishi

Wakati shule zikifunguliwa jana, baadhi ya wazazi wamelalamika watoto wao kurudishwa nyumbani kutokana na kushindwa kupeleka michango, inayojumuisha chakula na fedha kwa ajili ya posho ya mpishi.


Wakizungumza nasi kwa njia ya simu jana, wazazi hao walidai kutakiwa kupeleka mahindi debe moja kwa kila mtoto, maharage kilo tano na Sh. 9,000 kwa ajili ya mpishi na mafuta.

Mmoja wa wazazi hao, Daines Msigala, mkazi wa Magegele, Halmashauri ya Mji wa Makambako, alidai kupeleka mtoto wake shuleni, lakini alirudishwa kutokana na kukosa michango hiyo.

"Wanataka chakula shuleni, lakini changamoto kama mimi mwenyewe watoto wa darasa la awali, la kwanza na la pili wote nimetakiwa nitoe michango ya chakula.

"Kama huna chakula, huwezi kupokewa, kama huna mahindi na maharage, huna Sh. 9,000 huwezi kupokewa, mtoto wako unarudi naye nyumbani," alilalamika Msigala.

Alisema tangazo lililotolewa ni kila mwenye mtoto ambaye hajalipa michango arudi nyumbani.

Mzazi mwingine, Asifiwe Mponda alisema wamekwenda shuleni na mwanawe, lakini akaambiwa kama hawana mchango wa chakula warudi na watoto wao nyumbani.

Kutokana na changamoto ya maisha, aliomba wapewe muda ili watafuta michango hiyo," akifafanua: "Bora wangetusikiliza sisi wazazi hata kidogo tutalipa, hawana hata maelewano, tulikaa kikao wakasema kuanzia Januari watoto waje na chakula na fedha, tukakubaliana ila leo tumekwenda wazazi baadhi tulikuwa hatuna hivyo vitu.

"Tumeomba wiki hii tutatoa, hawataki. Kama hujalipa, rudi na mwanao nyumbani kajipigepige utakapopata chakula ndipo uje mwanao atapokewa," alidai Mponda.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Keneth Haule alipoulizwa na Nipashe kuhusu madai hayo, alisema inawezekana tatizo hilo la watoto kurudishwa nyumbani ni la kweli kwa kuwa amepokea malalamiko ya aina hiyo ofisini.

"Niliongea na mwalimu mkuu asubuhi, alinithibitishia kuwa hilo suala halipo,lakini niliwatuma watu wangu walikwenda huko Magegele na wenyewe walienda kuzikuta hizo changamoto na zoezi la uandikishaji linaendelea.

"Changamoto inaweza kuwa imetokea kwa mzazi mmoja, wawili kwa sababu suala hili la kurudisha watoto limeongewa sana na viongozi na Mkuu wa Mkoa kwenye vikao aliongea na vyombo vya habari vimeongea. Kwa hiyo, unakuta tatizo la mtu mmoja mmoja," alisema.

Hata hivyo, alisema badala ya kuchukua hatua ya kumrudisha mtoto nyumbani, wazazi ndiyo wawajibishwe kwa sababu walikubaliana kwenye vikao, lakini wakashindwa kutekeleza.

"Serikali za mitaa zipo, bodi za shule zipo, kamati za shule zipo wahangaike na mzazi siyo mtoto na nimewaambia kwenye taarifa yangu kwamba mnaposajili watoto na namba za wazazi mnasajili, mpigieni mzazi ikiwezekana mwombe aje shuleni mzungumze naye, siyo suala la kumrudisha mtoto, anahusiana na nini, aachwe aingie darasani," alisema Haule.

Akizungumzia madai hayo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Magegele, Amos Mtawa anayelalamikiwa, alisema suala la chakula linasimamiwa na kamati ya chakula ambayo inachaguliwa na wazazi.

"Utaratibu waliupanga wao kwenye kikao juu ya usimamizi wa ukusanyaji wa chakula. Watoto waliorudishwa siwezi nikalizungumzia maana sijatambua waliorudishwa ni kina nani, ni kosa limefanyika, nitalisimamia," alifafanua Mwalimu Mtawa.

KAULI YA WAZIRI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda, akizungumzia suala hilo mkoani Kilimanjaro jana, alisema ni marufuku kwa shule za serikali kuchangisha michango kwa lazima.

Prof. Mkenda alisema michango inayoruhusiwa ni ile ya hiari, akitamka: "Serikali imeondoa ada, sasa walimu baada ya kuona ada zimeondolewa, wameweka michango yao kwenye fomu za kujiunga na shule. Kuna watoto wanaacha kwenda shuleni kwa sababu ya hii michango.

"Michango hii ni mingi zaidi ya ile ada tuliyoiondoa. Tunahimiza wazazi wachangie kwa hiari na washirika wachangie lakini hakuna mchango wa lazima.

"Tumeshamwambia Kamishna wa Elimu atoe mwongozo wa kuzuia michango hii, asisitize hizi fomu za kujiunga na shule zinakwenda kinyume cha maelekezo ya serikali kwa kuweka michango ya lazima ambayo ni mingi zaidi kuliko ada iliyofutwa na serikali.

"Unamwambia mtoto ada imefutwa lakini unaweka michango inayofikia laki tatu (300,000/-), tutaanza kufuatilia hizi shule zenye michango hii inayokiuka miongozo, walimu wakuu tutawawajibisha, wakurugenzi wa halmashauri tutamshauri Mheshimiwa Rais waitwe na kujieleza kwanini wanaruhusu hali hii?"

Chanzo:Nipashe


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo