Wakili, Jebra Kambole amesema licha ya Serikali kuondoa zuio la mikutano ya hadhara vyama vya vya siasa vinapaswa kuombwa radhi kwa kutofanya shughuli zao kwa ufanisi kutokana na katazo hilo.
Katazo la mikutano ya hadhara lililowekwa na Serikali ya awamu ya tano mwaka 2016 ilikuwa kinyume na Katiba ya Tanzania, kwa sababu Katiba haijaweka ukomo kwa vyama vya siasa kutofanya siasa.
“Haikuwa sahihi kwa sababu vyama havikupata fursa ya kukua na kujitangaza, katazo lilikuwa kinyume cha sheria na Katiba. Vyama vina haki ya kuomba radhi kwa kilichotokea pamoja na ruhusa kutolewa ni hatua nzuri siyo jambo la kubeza na uthibitisho kwamba kilicholiliwa kilikuwa sahihi.
Januari 3, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu Ikulu Dar es Salaam, aliruhusu mikutano ya hadhara iiliyokuwa ikililiwa kwa muda mrefu na vyama vya upinzani kutaka ruhusiwe.
"Uwepo wangu leo (jana) hapa mahali nimekuja kufanya ruhusa ya mikutano hii, nimekuja kutangaza kuondoa zuio la kuzuia mikutano ya hadhara na ninasema kwamba, sasa linaondoka,” amesema.
Kambole amesema hayo leo Jumatano Januari 4, 2023 katika mjadala wa ‘Twitter Space’ uliokuwa na mada ya ‘kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara na kuukwamua mchakato wa Katiba je ni mwelekeo mpya wa siasa nchini?
Katika maelezo yake, Kambole amesema siasa sio uchaguzi tu, bali kusajili chama, kampeni, mikutano, akisema huwa aamini watu wanaosema nchi ikiwa inaajengwa siasa haziruhusiwi.
Amesema Sheria za vyama vya siasa, Sura namba 258 kifungu cha 11 kinaeleza vyama vilivyosjiliwa vina haki kufanya mikutano ya hadhara, haki ya kulindwa na vyombo vya dola, akisema ukizuia vitu vya namna hiyo unakiuka sheria.
Hata hivyo, Kambole amesema kuna ulazima kukatungwa kwa sheria za vyama vya siasa zitakazokuwa rafiki kwa vyama vya siasa ili kutekeleza majukumu ya shughuli za kisiasa kwa ufanisi tofauti na ilivyo sasa.
Chanzo: Mwananchi