MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho hususan vijana kukwepa siasa za ugomvi na matusi wanapofanya mikutano ya hadhara.
Akizungumza katika ufungaji wa matembezi ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), leo tarehe 10 Januari 2023 visiwani Zanzibar, Dk. Samia amesema siasa za aina hiyo zikome kwa kuwa hivi sasa nchi katika siasa za maridhiano na ustahimilivu.
“Sasa niwatake vijana pamoja na kutimiza malengo ya falsafa hiyo ya maridhiano, ustahimilivu na mabadiliko, sasa niwaambie kwamba zama za ugomvi, kupigana na kutukanana katika siasa sasa ziishe twendeni na hoja za maana za kujenga. Tuvumiliane tulete maendeleo ya kweli na yenye tija ili tuijenge Tanzania mpya yenye maendeleo endelevu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema “mtakapokwenda kupayuka mkajibu hoja za ovyo hapo huonyeshi uongozo, uongozi ni kuonyesha njia twendeni tukaonyeshe njia.”
Dk. Samia ambaye ni Rais wa Tanzania, amekitaka chama hicho kuvunja makundi kwa ajili ya kujiandaa na chaguzi zijazo “twendeni tukafanye mabadiliko ndani ya chama na jumuiya zetu, maugomvi yakome tunakwenda kwenye mapambano ya kisiasa, tunakwenda kutetea nafasi yetu ndani ya nchi. 2024 tuna uchaguzi wa TAMISEMI tukienda tumegawanyika hatutafanya vizuri.”
Mwenyekiti huyo wa CCM amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kufanyia kazi masuala yatakayokosolewa na wapinzani katika mikutano ya hadhara na kwa yale ya uongo wayapinge kwa kutoa ufafanuzi wa hoja.
“Sisi CCM tunajipanga, hivyo kuna vyama ambavyo vinajipanga hivyo watakuja na ya kwao kutukosoa. Naomba sana tunapokosolewa tuyaangalie yale ya kweli tuyachukue tuyafanyie kazi yawe makosa yameondoka. Yale ambayo si ya kweli twendeni tukajibu kwa hoja lakini kubwa ni ustahimilivu,” amesema Rais Samia.