Mbunge wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, Nicholas Ngassa, anatarajia kutumia kiasi cha Shilingi 480 Milioni, kwa ajili ujenzi wa ofisi za kata za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye kata 16 za jimbo hilo.
Ngassa aliyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi ramani ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) pamoja na matofali 1000 na mifuko ya sementi 100 wilayani Igunga jana. “Moja ya ahadi niliyoitoa kwa wanachama wa CCM jimbo la Iigunga wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ni kujenga ofisi za chama kwenye kata zote 16 jimbo la Igunga kwa fedha zangu binafsi.” Alisema.
Ngassa aliongeza kusema kuwa mpango huo wa ujenzi wa ofisi hizo upo tayari na unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni huku matarajio yakiwa ni kukamilisha ujenzi huo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“ CCM ni chama kikongwe na ni chama kikubwa kinachoaminiwa, kupendwa na kutegemewa na mamilioni ya watanzania. Ni lazima kiwe na miundombinu wezeshi itakayo warahisishia watendaji wake kufanya kazi kwa ufanisi”. Alisema Ngassa.
Ngasa alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa chama hicho kuendelea kujijenga kuanzia ngazi za chini, na kwa mapenzi makubwa aliyonayo kwa chama chake, ameamua kutumia fedha zake binfsi zinazotokana na mshahara wake na vyanzo vyake vingine vya mapato, kuhakikisha kuwa kata zote za jimbo hilo zinakuwa na ofisi ambazo zitakuwa na sehemu ya ukumbi wa mikutano na vyumba vitatu vya biashara.