Bondia wa Tanzania Karim Mandonga alithibitisha mbwembwe zake za kabla ya pambano kwa kumtandika mpinzani wake Mkenya Daniel Wanyonyi katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi.
Mechi hiyo ilivutia umati mkubwa wa watu kutokana na mbwembwe na mashauo ya Mandonga na kwa kweli waliohudhuria hawakukosa burudani kwani Mtanzania huyo alianza kurusha ngumi moto kutoka sekunde ya kwanza hadi pambano lilipomalizika.
Wawili hao walisukumana hadi raundi ya tano ambapo "Mtu Kazi" aliendeleza mashambulizi na kumfanya Wanyonyi kudinda kurejea kwa raundi ya sita - ushindi ukipewa Mandonga.
Ushindi huuu ni mkubwa wa Mandonga ambaye sasa amejihakikishia nafasi kama mmoja wa mabondia bora Afrika Mashariki. Bondia huyo amejitetea kwa mbwembwe zake akisema kuwa ndondi zinahitaji mdomo kuzitangaza na kuahidi kurejea nchini mwezi Aprili kwa pambano jingine. “Mdomo ni wa kupiga promo, nikiingia ulingo iko nafasi ya ngumi. Narudi tena Nairobi, Kenya hii Aprili ‘kumzika mtu’, raundi ya kwanza kaburi lake liko wapi? Muwekeni pale!" Mandonga alisema.