Kwa nini wenye ulemavu wa macho wanalilia kondomu za nukta nundu?


KWENYE moja ya vikao vya kamati ya watu wenye ulemavu nchini Tanzania, hoja iliyogusa hisia kubwa za wengi ni ya watu wenye ulemavu wa kuona kusisitiza uwepo wa mipira ya kiume (kondomu) yenye nukta nundu.


Kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa mwaka jana, huko nyanda za juu kusini katika mkoa wa Mbeya kilikuwa na lengo la kujadili changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu wa aina zote na kuweka maazimio ya kukabiliana nazo kwa mwaka mpya.


Kilio hiki cha kutaka kondomu za nukta nundu hakijaanza leo wala jana na hakijaanzia kwa watu wenye ulemavu Tanzania, ni kilio cha muda mrefu kutoka kwa watu wenye ulemavu wa kuona kutoka karibu nchi nyingi za Afrika.


Swali kubwa hapa kwanini watu hawa wanahitaji kondomu hizi za nukta nundu?

NUKTA NUNDU NI NINI?

Nukta nundu ama Braille ni mfumo wa herufi zinazoshikika au kutambulika kwa vidole ambapo herufi hizo, namba au alama za kisayansi zinachapishwa kuwasaidia watu wasioona au wenye uoni hafifu kutambua na kusoma vyema kama watu wengine.


Mfumo huu uligunduliwa katika karne ya 19 na mfaransa Louise Braille. Akiwa na umri wa miaka 3, alipata tatizo la jicho moja ambalo baadaye lilisambaa na kuharibu na jicho lingine.


Alikuwa moja ya watoto wenye akili sana darasani licha ya matatizo yake ya macho. Akafanikiwa kupata ufadhili wa masomo kutoka serikalini. Akiwa masomoni aliendelea kufikiria kugundua mfumo ambao utawasaidia watu wenye ulemavu wa macho kuweza kutambua na kusoma herufi.


Akiwa na miaka 15 kwa mara ya kwanza akaja na mfumo huu akiwasilisha kwa vijana wenzake mwaka 1824 na ukaonekana ni mfumo mzuri.


Huo ukawa mwanzo wa maandishi ya nukta nundu yanayotumika duniani kote na ndiyo yanayofundishwa shuleni, mfumo huu ukipewa jina lake Braille.


HOJA YA KONDOMU ZA NUKTA NUNDU INAVYOPAA AFRIKA

Kwa sasa katika maeneo mengi bidhaa zenye maaandishi ya nukta nundu zinaanza kuzalishwa kwa wingi hasa Ulaya. Kwa mfano bidhaa za dawa mbalimbali za binadamu, vitabu, vifaa vya umeme vimekuwa na maandishi ya nukta nundu.


‘Ni muhimu sana hili, si la kulitazama kawaida, kwetu tusioona ni muhimu sana’, anasema Moses Kaisa, mlemavu wa macho kutoka Dar es Salaam.


Japo si kwa wingi huo, lakini kuanza kuenea kwa bidhaa za namna hiyo, kunaanza kutoa msukumo kwa watu wenye ulemavu wa macho kutaka pia kuwe na kondomu zilizochapishwa maandishi ya nukta nundu.


Mwaka 2021, Taasisi moja inayoitwa Botswana Family Welfare Association (BOFWA), ya nchini Botswana, iliamua kutengeneza kondomu za nukta nundu ‘braille condom’.


Haikuishia hapo ilijiingiza mpaka Namibia kwa lengo la kushawishi uzalishaji wa kondou za aina hiyo kwa ajili ya watu wasioona ama wenye uoni hafifu.


Hiyo iinatajwa ilikuwa ni mara ya kwanza katika ukanda wa kusini mwa janga la Sahara, kwa taasisi ya aina hiyo kujitokeza hadharani kupigania kondomu za nukta nundu kwa usalama wa afya ya walemavu wasioona.


‘nimefuatilia wenzetu wameanza, sio Ulaya tu huko utasmea mbali, hapa Afrika,Botswana wameonyesha mfano’, alisema Kaisa


Nchini Uganda hoja hii ya kondomu za nukta nundu zilipigiwa makelele muda mrefu tanhu miaka ya 2000. Na jamii ya watu wasioona huko Gulu, ilikuw amstari wa mbele.


Mwaka 2008 msemaji wa jamii hiyo, Robert Opiyo alinukuliwa akisema walemavu wanapaswa kupewa huduma za kipekee kulingana na mahitaji yao, na kondomu za nukta nundu ni hitaji lao la msingi.


KWANI NINI KONDOMU ZA NUKTA NUNDU NI MUHIMU KWA WALEMAVU?

Kondomu ni kinga dhidi ya magonjwa ya zinaa (STD’s). Kama ni bora na haijakwisha muda wake, wataalamu wanaipa nafasi kubwa kondomu ya kukulinda dhidi ya magonjwa kama Ukimwi, kisonono, kaswende na magonjwa mengine.


Lakini inaweza kuzuia mimba zisizopangwa na inatumika kama moja ya njia ya uzazi wa mpango. Kazi hizo za kondomu zinawajibika ama kuwagusa watu wote awe mlemavu wa macho ama asiye mlemavu wa macho.


‘Walemavu ni binadamu kama wengine na wana mahitaji, kwa hiyo kama wakiweka (nunda nundu kwenye kondomu) itapendeza’, anasema Sylvanus Hosea, mwalimu mstaafu na mlemavu wa macho kutoka Dodoma.


Anaungwa mkono na Kaisa anayesema ‘ tuko kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa magonjwa, kwa sababu wengi tunashindwa kutambua kama mipira (kondomu) ime-expire (imekwisha muda wake wa matumizi) ama la, kwa kuwa hatuwezi kusoma’.


Hili la kuwa kwenye hatari ya kuambukizwa ndilo linalowaweka njia panda walemavu wa macho na kutaka kondomu za nukta nundu ili kulinda afya zao.


Lakini Hosea ana mashaka kama linaweza kuwa suluhu la kudumu kw awatu wasioona ‘Kama wanaoona tu wanatumia kondomu zilizokwisha muda wake, sie je? ‘ Tusifikirie kwamba wakiandika (maandishi ya nukta nundu kwenye kondomu) tutakuwa tumetatua matatizo yote ya watu wasioona kutumbukia kwenye hatari hiyo (maambukizi ya magonjwa), Je walemavu ambao hawakwenda shule na hawajui kusoma maandishi ya nukta nundu? anahoji Hosea.


Pamoja na hoja za Hosea, Ibara ya 21 na 24 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu(CRPD) inataja nukta nundu kama mbinu ya kusaidia ujumuishaji kwenye jamii kwa watu wasioona na wenye uoni hafifu.


Kilio cha watu hao ni haki inayotambuliwa kimataifa na nukta nundu inatambulika pia kwenye mkataba huo Ibara ya 2 pamoja na mambo mengine kama mbinu muhimu kwenye uhuru wa kujieleza kupata taarifa na mawasiliano mbalimbali.


Mchapisho ya nukta nundu kweye kondomu zitawapa taarifa, lakini ni kwa kiasi gani hilo linaweza kutekelezeka? huu bado ni hoja pana inayohitaji mjadala mpana. Makala hii imeandaliwa na kwa msaada wa mtandao wa BBC.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo