Kijiji cha Usagatikwa wilayani Makete mkoani Njombe kipo kwenye hatari ya kukosa wasomi katika siku zijazo kutokana na wanafunzi wanaopangiwa kuanza kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Lupalilo wengi wao kutohitimu kidato cha Nne
Akitoa taarifa ya ripoti ya wanafunzi wa kidato cha
kwanza 2023 katika Kikao cha kamati ya Maendeleo ya Kata ya Tandala kwa robo ya
pili Januari 16, 2023 Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Lupalilo Mwl.
Lunanilo Kilatu amesema hali haikuwa nzuri Ijumaa ya wiki iliyopita kwani
walikuwa wameripoti kwa asilimia 44 hali iliyopelekea taarifa kutumwa kwa
mtendaji wa kata lakini hadi kufikia jana asubuhi kumekuwa na ongezeko la
wanafunzi walioripoti kwa asilimia 73 kwani kiujumla wamesharipoti wanafunzi 91
kati ya 124 waliopangwa kwenye shule hiyo
Mwalimu huyo amesema kumekuwa na changamoto ya wanafunzi hao baada ya kuripoti shuleni kusema kuwa hawataki kusoma jambo ambalo ameomba ushirikiano kwa serikali na wazazi kuwadhibiti watoto wao ili wasome kwao wao kama shule wamewakatalia na kuwaambia kuwa hakuna mtoto atakayeacha shule
Kaimu Mkuu huyo wa shule hakusita kuzungumzia suala la
wanafunzi wanaopangiwa shuleni hapo kutoka kijiji cha Usagatikwa kutoripoti
shuleni na hatari ya kijiji hicho kukosa wasomi
Hali hiyo ya kijiji cha Usagatikwa imeungwa mkono na Afisa Elimu Kata ya Tandala Mwl. Eskaka Sanga ambapo amelazimika kutoa takwimu za matokeo ya kuhitimu elimu ya msingi 2022 kwa shule za kata yake ambapo kwa Tandala walifanya mtihani watoto 40 wakafaulu 37, Ihela walifanya mtihani wanafunzi 25 wakafaulu 23, Ikonda walifanya mtihani 56 waliofaulu ni 53 na kwa Usagatikwa walifanya mtihani wanafunzi 33 na wakafaulu 14 sawa na asilimua 42 ambapo ukilinganisha na mwaka juzi Usagatikwa walifanya mtihani watoto 26 na wakafaulu 13
Afisa Elimu huyo amesema katika utafiti walioufanya
katika kijiji hicho pamoja na sababu zingine za walimu lakini wamebaini kuwa
tatizo lipo kwa wazazi kwani wanafunzi hao wamekuwa wakifanya vizuri mitihani
yao mingine lakini wanashawishiwa na wazazi wafanye vibaya kwa kuwa baadhi ya
wazazi hawapendi watoto wao wasome na pia wale wanaofaulu kujiunga na kidato
cha kwanza utafiti umeonesha wawili ndio wanaohitimu kidato cha nne ama wakati
mwingine wasiwepo kabisa
Sauti Mbilinyi, na Mwl. Josephat Nuje ni miongoni mwa washiriki wa kikao hicho cha KAMAKA na kutoa maoni yao kuhusu suala hilo la elimu na kuelezzea masikitiko yao kuhusu wazazi wanafumbia macho vitendo hivyo
Mwenyekiti wa Kijiji Cha Usagatikwa Albeto Sanga amesema wao tayari wamejipanga kuchukua hatua kwa wazazi wanaoshindwa kuwapeleka watoto shule na wale wanaowashawishi wafeli
Kikao hicho Kimekubaliana majina ya wanafunzi ambao hawajaripoti kidato cha kwanza na waliotoroka shule miaka iliyopita ambao wanatakiwa kuwepo shule sasa hivi yawasilishwe kwa mtendaji wa Kata kwa hatua zaidi huku pia wenyeviti wa vijiji wakitakiwa kuwasilisha mapema taarifa za mikutano yao ya kijiji ili viongozi wafike kutoa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa watoto wao kwenda shuleni