Mwili wa Kijana Nelson Mollel ambaye alifariki dunia katika Kata ya Moivo, Sanawari Wilayani Arumeru Mkoani Arusha kwa madai ya kuchapwa fimbo 70 za jamii ya Kimaasai hatimaye umezikwa Jumatatu, Januari 16, 2023.
Nelson alipigwa fimbo hizo kwa madai ya utovu wa nidhamu ikiwemo kumtukana mama yake mzazi na kumkana.
Vijana wengi ambao ni marafiki wa marehemu wamejitokeza kumsindikiza mwenzao huku familia yake ikishangaa kitendo cha vijana hao walipokuwa wanazika kwa kutumia mikono badala ya kutumia beleshi (sepetu).
Richard Mollel ambaye ni Mzee wa Ukoo wa familia amesema vijana hao wametoa taswira mbaya na kufanya fedheha kwa kuwa familia haiwafahamu vijana hao.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishina Msaidizi wa Polisi ACP. Justine Masejo amesema Jeshi la Polisi wanachunguza tukio hilo na kuwasaka wote waliohusika ili kufikishwa kwenye vyombo vya dola.