Ilichokifanya Taasisi ya Sauti ya Mama Afrika Huko Mbeya





Na Kenneth Ngelesi,Mbeya


TAASISi ya Sauti ya Mama Afrika Foundation(SAMAFO) imekuwa Taasisi ya kwanza Mkoani Mbeya kuitikia wito wa kutoa msaada wa nguo kwa ajili ya maafa yaliyotokana na mafuriko Kata za Iduda,Uyole,Iganjo, Nsalaga na Igawilo yaliyotokea januari 7, Mwaka huuu ambayo yamesababisha madhara kwa baadhi ya wananchi wa kata hizo.

Akikabidhi msaada huo mbele ya kamati ndogo ya maafa Mkoa wa Mbeya Mkurugenzi wa SAMAFO Tabitha Bugali amesema wameguswa na maafa hayo baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari.

Bugali amesema baada ya kupata taarifa za mafuriko walilazimika kukusanya nguo za watoto,wanaume na wanawake aina mbalimbali kwa ajili ya kusaidia wahanga.

Kwa upande wake Katibu wa SAMAFO Hidaya Marekani amewashukuru wanachama wote waliochangia msaada ambao wameuwakilisha Mkoani kwa ajili ya kusaidia wahanga.

Akipokea msaada huo Mwenyekiti wa kamati ndogo ya maafa Mkoa wa Mbeya Erick Sichinga ameishukuru Taasisi ya SAMAFO kwa namna walivyojitokeza kutoa msaada huo na kwamba bado msaada mkubwa unahitajika ili kuwasaidia wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo.

Aidha amesema misaada yote inapokelewa na kamati yake na itashirikiana na kamati mama inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye atakabidhi wilayani ili kuwafikia walengwa.

Sichinga ametoa wito kwa Taasisi na mashirika kujitokeza kutoa msaada wa hali na mali na kwamba nguo,vyakula na mablanketi vinahitajika ili kukabiliana na maafa kwa kuwa bado mvua zinaendelea kunyesha.

Katibu wa kamati ndogo ya maafa Mkoa wa Mbeya Juma Maduhu amesema kamati yake haipokei fedha taslim bali hupokea vitu na vyakula ambavyo vitatolewa kwa utaratibu maalum utakaopangwa na kamati mama.

Naye Mohammed Mkindi Afisa Tawala Mkoa wa Mbeya amesema misaada umekuja kwa wakati ambao utasaidia kupunguza makali kwa wahanga wa mafuriko.

Kutokana na mafuriko hayo baadhi ya kaya zimebomokewa na nyumba zao vyakula kuharibiwa sambamba na wanafunzi waliosombewa sare vitabu na madaftari.

Kata ya Uyole ndiyo iliyopata athari kubwa zaidi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson ametoa mchele na maharage huku akishauri kuboreshwa miundombinu hususani usafi wa mitaro jijini Mbeya.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo