Katika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania bara), Halmashauri ya wilaya ya Makete Mkoani Njombe imefanya kongamano la kujadili mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo hasa kuimulika Makete kwa miaka 61 ijayo.
Kongamano hilo limefanyika leo Desemba 9, 2022 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, na
kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wazee na wadau
mbalimbali wa maendeleo
Awali kabla ya ufunguzi wa kongamano hilo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Makete William Makufwe ametoa taarifa
fupi juu ya historia ya wilaya ya Makete tangu kuanzishwa kwake mpaka sasa.
Makufwe amesema kwa sasa Wilaya ya Makete imepiga hatua za kimaendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji, na miundombinu ya barabara
Mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda ndiye
aliyekuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano hilo, akizungumza na washiriki amesema siku
ya kumbukizi ya uhuru ni muhimu kwa kuwa inaweka historia kwa vizazi na vizazi
kuhusu ukombozi uliofanywa na waasisi wa taifa hili kwa manufaa ya watanzania
wote huku akisisitiza umuhimu wa kutunza amani tuliyonayo
Baada ya mgeni Rasmi kufungua kongamano hilo, baadhi ya washiriki mbalimbali na viongozi wa serikali waliohudhuria akiwemo Mwalimu Remijo Tweve kutoka shule ya msingi Mahulu Kipagalo, Frida Sanga na Mchungaji Denis Sinene wamezungumzia miaka 61 ya Uhuru kwa wilaya ya Makete kwa kukiri kuwa kuna mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yaliyofanyika tangu uhuru mpaka sasa