Taarifa zilizozagaa kwenye
mitandao ya kijamii kuhusu mtu kuweka sumu kwenye kisima cha maji wanachotumia
wananchi wa Kijiji cha Mlondwe wilayani Makete mkoani Njombe, zimeifanya
serikali kupitia katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kufika na kutoa taarifa
sahihi za tukio hilo
Leo Desemba 10,2022 Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga amefanya ziara ya kikazi kijijini hapo ambapo amesema walipata taarifa hizo zilizokuwa zikienezwa kwenye mitandao ya kijamii na kulazimika Wizara kutuma timu ya wataalamu wa maabara kufika hapo na kufanya uchunguzi wa kimaabara wa maji hayo ili kubaini kama yana sumu au lah kwani zinapotolewa taarifa kama hizo bila kujali ni za kweli au si za kweli wao ni lazima watume wataalamu ili wajiridhishe
Mhandisi Sanga amesema baada
ya timu ya wataalamu kupima maji hayo katika maabara imeonekana hayana sumu
hivyo wananchi waendelee kuyatumia na hawana haja ya kuwa na wasiwasi na
taarifa hizo zinazoenezwa kuwa maji hayo yana sumu, kitu ambacho si kweli
"Tulipopata sisi hii
taarifa pia moja ya sababu ya kuja huku pia ilikuwa ni kufuatilia hili lakini
pia bahati nzuri tulituma wataalamu wetu kutoka Iringa wa maabara na
wamenitumia taarifa sasa hivi ninavyoongea bahati nzuri taarifa nimeshaipata na
ni kweli tukipata taarifa yeyote sisi lazima tupime yaani hata kama ni ya kweli
au uongo yakishazungumzwa tu lazima tukajiridhishe kama pana ukweli au hamna
ukweli, ukweli ni kwamba hakuna sumu pale, kwa hivyo kama tulivyoongea toka
mwanzo tujitahidi sana kutoleta taharuki kwa wananchi sio vizuri, unapoongelea
sumu ni changamoto kubwa sana inaweza kuleta taharuki watu wakapigana
wakaumizana jambo ambalo sio zuri sana, kwa hiyo maji yale imeonekana hayana
sumu kwa hiyo yale matumizi mliyopanga
kuyatekeleza endeleeni kuyatumia hayana shida yoyote" amesema Mhandisi
Sanga
Diwani wa Kata ya Mlondwe
Alphonce Salimo akizungumzia suaa hilo amesema nao walibaini ni la uzushi na
halina ukweli wowote kwani kulikuwa na ugomvi binafsi baina ya aliyetoa taarifa
na anayetuhumiwa kuwa aliweka sumu kwenye chanzo cha maji, na hiyo ilitokana na
kushindwa kesi waliyokuwa nayo kwenye baraza la ardhi, hivyo akaona atumie njia
hiyo kumchafua mwenzake
"Nataka nikuhakikishie
kama diwani wa eneo hili ni uongo na hakuna ukweli wowote kwenye hayo mazingira
ambayo ameyarusha kwenye Whatsappna kwenye magroup (makundi) lakini nikuombe
kwa sasa kwenye kata yetu hii kuna watu wanadhani kule kwenye magroup na kwenye
whatsapp kusema uongo kwa mambo ambayo sio ya ukweli wanaona ni mambo ya
kawaida kwenye kata hii, kwa hiyo nikuombe Katibu mkuu hata wakati mwingine
mtakapoyakuta haya kama ulivyofika leo Site (eneo la tukio) nadhani itapendeza
zaidi kwa sababu leo umejionea kwa macho ndio tunakueleza ukweli hayana ukweli
wowote ni uongo wao walikuwa wanagombana habari za mashamba na huyo alishindwa
kufuatana na sheria zilizotumika kwenye baraza la ardhi" amesema Diwani
Salimo
Mkuu wa wilaya ya Makete
Juma Sweda ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kisheria
kwa aliyehusika na utoaji wa taarifa hiyo ya uongo kwenye mitandao ya kijamii
kwa kuwa ripoti ya wataalamu wa maabara imeeleza ukweli halisi
"Bahati nzuri
tunawashukuru na vyombo vya dola mlianza kuchukua hatua na ninyi za kuanza
kuchunguza na bahati nzuri ripoti imetoka kwa sasa wale ambao walikuwa
wanadanganya kwa kutumia mitandao vibaya mshughulike nao, ili hii tuiondoe, kwa
sababu ripoti sasa ya kitaalamu
imeshatoka na mtu ameamua kutangaza kuleta taharuki kwenye maeneo yetu
yaani ishu za kiusalama zinaonekana kama ni tete fulani hivi unaogopa hata
kunywa maji unaweza kushinda una kiu haujanywa maji, sasa na ninyi watu wa
vyombo vya usalama sasa mshughulike na hicho kitu, huyu aliyepost kwenye
mtandao bila uhakika, bila kuwa na ripoti, bila kuwa na prove
(uhakika/uthibitisho) kwamba hiki kitu ni kweli, unaamua tu kurusha utengeneze
taharuki kwa wananchi kionekane kitu kikubwa lakini kumbe sio kitu
kikibwa" amesema Mkuu wa Wilaya
Amewataka watu kutumia
vizuri mitandao ya kijamii kwa kutoa taarifa sahihi na za ukweli badala ya
kutoa taarifa za kuzua taharuki huku akiahidi kufanya ziara siku za karibuni
kwenye kijiji hicho
"Mitandao tuitumieni
vizuri kwa ajili ya kujiletea maendeleo tuitumie vizuri kwa ajili ya
kuwasiliana na wapendwa wetu sio kuleta mambo yako ya ndani au mambo yako ya
ugomvi wewe na mtu kuyaleta, una shida naye ndio maana tuna vyombo vya dola,
una shida naye nenda kwenye vyombo vya dola watakusaidia, matokeo yake
itaonekana kijiji hiki ni kitukutu yaani kuna kipindi nilikuwa nasema hawa jamaa
ukiwapelekea mradi si watagombana? lakini kumbe kuna kagroup (kikundi) ka watu
wachache ambacho kanaendesha hivyo vitu, kwa hiyo hebu wazee kaeni nao muwaase
lakini na sisi serikali isiishie hapo mchukue hatua sasa za ziada pale kwa
sababu na ripoti nyie mnayo mchukue hatua ili tukomeshe haya mambo haya, rusha
kwenye mtandao kitu ambacho una uhakika nacho" amesema DC Sweda
Desemba 8, 2022 kwenye
mitandao ya kijamii hususan Whatsapp kwenye kundi la Mlondwe Ward Online
iliwekwa taarifa ikidai kwamba kuna chanzo cha maji ya kisima ambacho wananchi
wanakitumia kimewekwa sumu na viongozi wa kata hiyo wakilifumbia macho suala
hilo, jambo lililozua hali ya sintofahamu kwa wananchi na viongozi kwa ujumla
na kusababisha mamlaka zinazohusika kuanza kulishughulikia suala hilo ikiwemo
kutuma wataalamu waliofika kijijini hapo kufanya uchunguzi na vipimo vya
maabara na kutoa taarifa kwamba maji hayo hayana sumu.