Jeshi la Polisi mkoani Kagera limeanza uchunguzi wa kubaini watu wasiofahamika waliohusika na wizi wa mtoto mchanga wa kike Benita Beneti mwenye umri wa mwezi mmoja, ambaye anadaiwa kuibwa Desemba 1, 2022 majira ya usiku, katika mtaa wa Migera kata ya Nshambya katika manispaa ya Bukoba.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, William Mwampaghale amesema kuwa siku ya tukio majira ya saa moja usiku mama huyo Johanitha Augustino alitembelewa na marafiki zake watatu ambao aliwahi kuishi nao zamani katika mtaa wa Omukigusha kwa lengo la kumsalimia, na kwamba baada ya kumsalimia waliaga kundoka na baadae wawili walirejea kwa mama huyo na kudai wana mazungumzo naye.
"Mama huyo alikataa na kuahidi kufanya mazungumzo hayo kesho yake tarehe 02/12/2022 majira ya mchana, ndipo watu hao wakamuomba awasindikize, mara baada ya kuwasindikiza alirejea chumbani kwake hakumkuta mtoto wake aliyekuwa amelala kitandani, ndipo alipobaini kuwa ameibwa" amesema RPC Mwampaghale.