Sherehe ya harusi kati ya Swadiku Abas (50) na mke wake, Elieth Rwegashora (40) ambao ni wakazi wa Mtaa wa Zenze eneo lililopo Kiseke wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, iligeuka msiba baada ya bwana harusi kujinyonga muda mfupi kabla ya sherehe kuanza.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani hapa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jumamosi Desemba 24, 2022, tukio hilo lilitokea Desemba 17, 2022, muda mfupi baada ya wawili hao kufunga ndoa katika msikiti wa Swadikul Amiin.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa imeeleza kwamba sherehe ya ndoa hiyo iliyoingia dosari ilipangwa kufanyika katika ukumbi wa Mtena B lililopo eneo la Buzuruga jijini Mwanza na wakati taarifa za kifo hicho zinapatikana, ndugu, jamaa, marafiki na waalikwa tayari walikuwa ukumbinini.
“Baada ya kufunga ndoa, Desemba 17, 2022, wawili hao ambao tangu awali walikuwa wanaishi pamoja walitarajia kufanya sherehe katika ukumbi wa Mtena B, Buzuruga lakini mpaka Saa 4:00 usiku bwana harusi hakuonekana ukumbini, ndipo juhudi za kumtafuta zilipoanza,” inasema taarifa hiyo na kuongeza:
“Ilipofika Saa 5:45 usiku zilipatikana taarifa kwamba Swadiku Abasi amekutwa amejinyonga ndani kwake akitumia mtandio alioufunga kwenye kenchi la paa. Askari polisi walifika nyumbani hapo na kufanya uchunguzi wa awali ambapo kulipatikana kipande cha karatasi chenye ujumbe ambao umehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi na upelelezi."
Kutokana na mazingira ya tukio hilo, Jeshi la Polisi limewataka ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kuwa watulivu wakati upelelezi wa kifo hicho ukiendelea.
Kamanda Mutafungwa amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospital ya rufaa ya mkoa ya Sekou-Toure kwa uchunguzi wa kitaalam na upelelezi kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.