Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga amesema Serikali imetoa fedha shilingi Milioni 200 kukabiliana na tatizo la uhaba wa Maji katika kijiji cha Tandala Kata ya Tandala Wilayani Makete mkoani Njombe.
Mhandisi Sanga
leo Desemba 30, 2022 amefika kijiji cha Tandala na kukutana na viongozi wa
Kijiji hicho ambapo amesema fedha hizo zitaondoa tatizo la Maji kwa wananchi wa
vitongoji vya Posta na Singida ambao wamekuwa wakipata maji kwa Mgao na
kusisitiza kuwa Tandala inapaswa kupata maji kwa 100% na siyo asilimia 80 au
90.
Katibu Mkuu huyo amewasisitiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Makete (RUWASA) kuhakikisha mradi wa ujenzi wa Chanzo cha maji na usambazaji mabomba kijijini hapo unafanyika kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Januari 2023 hadi Aprili 2023 ili wananchi waanze kupata huduma hiyo huku akiahidi kuwa Serikali itatoa mita100 ili kuanza zoezi la ufungaji wa mita hizo kwenye makazi ya watu.
Awali Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Makete Martin Luvanda ameeleza namna ambavyo RUWASA wanaweza kujipanga kukabiliana na uhaba wa Maji Kijiji cha Tandala kwa ujenzi wa Chanzo, kufanya ukarabati wa miundombinu iliyopo na wamepanga kununua mita 500 za Maji ili kuzifunga kwenye makazi ya watu
Maurisia Sanga
na Chesko Kitumbika ni Wananchi wa Kijii cha Tandala waliozungumza na
mwanahabari wetu wameeleza adha wanayokutana nayo hivi sasa kufuatia kupata
maji kwa Mgao huku wakiishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo Milioni 200 ili
kusaidia upatikanaji wa huduma hiyo muhimu isiyokuwa na mbadala.