Serikali imewatoa hofu Watanzania kuhusu taarifa za kushikiliwa kwa ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) nchini Uholanzi, ikisema haiwezi kutaifishwa kutokana na rufaa ya kesi inayoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti kuhusu mwekezaji wa Sweden aliyeshinda tuzo ya Dola milioni 165 (TZS bilioni 380) dhidi ya Tanzania na kuishawishi Mahakama ya Uholanzi kushikilia ndege hiyo kama kigezo cha kushinikiza malipo yake, licha ya kutopata uhalali wa ICSID.
Akizungumza na gazeti laThe Citizen, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Feleshi amekiri mwekezaji huyo kushinda tuzo hiyo na ndege imeshikiliwa nchini humo.
“Ni kweli kwamba walienda katika mahakama ya nchini Uholanzi baada ya sisi kufanikiwa kubishana na ICSID ili kusitisha utekelezaji, lakini kila kitu kiko chini ya udhibiti,” amesema.
Kituo hicho cha ICSID chini ya majaji watatu, Sir Christopher Greenwood KC wa Uingereza, Stanimir Alexandrov na Funke Adekoya SAN kilitoa tuzo kwa niaba ya Eco-Development na kuamuru Tanzania kulipa kiasi hicho cha fedha Aprili mwaka huu.
Dkt. Feleshi amesema Serikali tayari imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya Uholanzi na kwamba hawezi kueleza mengi juu ya suala hilo.