Msemaji wa Serikali acharuka sakata la mabehewa kuwa ya mtumba

Siku chache baada ya mjadala mkali kutrendi kwenye mitandao ya kijamii juu ya mabehewa 14 yaliyonunuliwa na Serikali kuwa ni ya mtumba na kwamba thamani yake ni kubwa kuliko uhalisia, hatimaye Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa, ameibuka na kutolea ufafanuzi sakata hilo.


Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Msigwa alianza kwa kukazia kauli yake aliyoitoa jana akieleza kuwa mabehewa yaliyoingia nchini ni mapya na si mtumba kama ilivyoelezwa mitandaoni na wadau mbalimbali akiwemo mbunge wa Nzega Vijijini, Hamisi Kigwangalla.

Alisema, mabehewa hayo 14 ni mapya ambayo ni kati ya 59 yanayotengenezwa Korea Kusini na yalianza kutengenezwa tangu mwaka 2020 na mwaka huu, yameanza kuwasili.

Alisema, katika mabehewa 59 Serikali imeyanunua kwa dola milioni 55.6 na sio Dola Milioni 59.

“Ukipiga hesabu kwa wastani wa bei kwa behewa moja jipya ni kama dola 942,373, haya ni mabehewa mapya na hizi Serikali imenunua kwa utaratibu kwa kutumia utaratibu wa manunuzi,” alisema Msigwa.

Akizidi kufafanua juu ya mkanganyiko uliojitokeza ya kwamba Rais Samia alisema mabehewa hayo ni ya mtumba, Msigwa alisema, mabehewa ya mtumba ambayo Rais aliyazungumzia bado hayajafika.

“Hayo ni mabehewa 30 na vichwa 2 ambavyo tuliagiza kutoka Ujerumani bado hayajafika, na hayo ni ya ghorofa. Tunatarajia yatafika nchini Januari au Februari mwakani,” alisema Msigwa.

Msigwa alimaliza kwa kusema, mbali na mabehewa mapya 59 ambayo Serikali imeyaagiza kutoka Korea Kusini, Serikali imeagiza vichwa vingine 17 kutoka nchini humo na kwamba huku mabehewa mengine 1430 ya mizigo yakiagizwa kutoka nchini China ambayo bado yanatengenezwa na hayajafika nchini.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo