DC Simalenga afunguka madai ya kumshushia kipigo mwanafunzi


Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, limeanza uchunguzi wa madai ya Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Simon Simalenga, kumshambulia kwa kumpiga ngumi msichana Florencia Mjenda na kumsababishia jeraha kwenye jicho la kulia, kwa kosa la kukaa katika jukwaa lisilosahihi.


Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe 6 Desemba 2022 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, ACP Alex Mukama, baada ya video fupi inayomuonyesha msichana huyo akilalamika kushambuliwa na Simalenga, kusambaa mitandaoni.

Kamanda Mukama, amesema uchunguzi wa tukio hilo ukikamilika, taarifa itatolewa kwa umma.

“Na sie tumeliona hilo, tunalifanyia uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa kwenye vyombo. Lakini tuna taarifa ya tukio hilo tumeliona sidhani kama liko kama ilivyoelezwa,” amesema Kamanda Mukama.

Katika video hiyo fupi, Florencia alidai tukio hilo lilitokea wakati yeye na wenzake walipokwenda kushiriki michezo ambapo walikaa katika jukwaa ambalo si sahihi, ndipo Simalenga alipowaita ambapo yeye alikwenda kumsikiliza kisha akaanza kumpiga.

Florencia anadai kuwa, baada ya Simalenga kuanza kumpiga alimuomba msamaha akimueleza yeye ni mgeni hivyo hakujua kama jukwaa hilo halikuandaliwa kwa ajili yao.

Hata hivyo, Simalenga amekanusha madai hayo akisema hakuna mtu aliyepigwa bali alitoa maelekezo.

“Hakuna mtu aliyepigwa kwa namna ambavyo imeelezwa, mimi nilichofanya ni kutoa maelekezo. Nilimshika mkono na aliniomba msamaha,” amedai Simalenga.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo