MTANDAO wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi umepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kucharazwa viboko wanawake wakongwe mkoani Tabora na kutoa mapendekezo matano ili kukomesha
Tayari Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum jana Desemba 15, 2022 aliielekeza ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora kwa niaba ya Kamishna wa Ustawii wa Jamii, kushirikiana na vyombo vya haki mkoani humo kuhakikisha wanafufua shauri la wazee hao waliochapwa viboko kwa tuhuma za kishirikina, ili mashahidi watoe ushahidi wao kuhusu kesi hiyo.
Hata hivyo, Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi katika taarifa yao iliyotolewa leo Desemba 16, 2022, imesema pamoja na kuipongeza serikali kwa hatua ilizozichukua kufuatilia suala hilo kupitia Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; bado kuna haja ya suala hilo kuwekewa msisitizo na hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wanaokwamisha upatikanaji wa haki kwa ukatili mkubwa uliotendeka.
“ Tunatoa wito kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufanya upelelezi kwa wale wote waliohusika katika tukio hili la kinyama na la kusikitisha,”imesema taarifa hiyo
Aidha, wameomba kuwarejesha wanawake hao katika makazi yao pamoja na kuwapatia ulinzi.
“Pia tunashauri suala hili lifuatiliwe na kushughulikiwa kwa uwazi ili wananchi wote waweze kurejesha imani ya utawala wa sheria na upatikanaji wa haki kwa viongozi na serikali kwa ujumla.” Imesema taarifa hiyo ya Wanamtandao na kuongeza
“Mtandao unaendelea kutoa wito kwa jamii kutovifumbia macho vitendo dhalilishi, vya kikatili, vya kinyama na vya uvunjifu wa haki kwa wanawake na jamii nzima, kuchukua hatua na kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi vitendo hivyo vinapofanyika.” Imesisitiza
Tamko hilo la Wanamtando limekuja ikiwa ni siku moja baada ya kusambaa video kulisambaa ‘clip ya video’ inayowaonyesha wanawake wakongwe wanne na binti zao wawili mmoja akiwa mjamzito, wamechapwa viboko wakiwa wamemwagiwa maji na kupunguzwa nguo mwilini.
Video hiyo ilionesha wanawake hao wakilalamika kitendo hicho ambacho kinadaiwa kufanywa na baadh ya watu kwa kushikiriana na Diwani wa Kata ya Kasisi, Wilaya ya Urambo, Mkoa wa Tabora kwa madai kuwa wanawake hao ni wachawi na washirikina ambao wamekuwa wakichukua vyakula vya watu kwa nguvu za kishirikina wakati wa usiku.
Wanawake hao walipatwa na kadhia hiyo wakiwa katika shughuli zao za kujipatia kipato ambapo kufuatia tukio hilo walipoteza mazao na vitu mbalimbali. Tukio hilo pia liliwasababishia maumivu makali ya mwili na viungo, limewadhalilisha wao binafsi, familia zao na jamii nzima.
“Mpaka taarifa hizi zinatufikia, tayari familia za wanawake hao zilikuwa zimelazimika kuhama makazi na kwenda kuishi maeneo mengine kwa kuogopa vipigo zaidi, kubomolewa nyumba zao na vitisho dhidi ya maisha yao ambavyo walivipata kutoka kwa Diwani huyo. Mtandao unajiuliza, Je usalama wa hawa watu uko wapi? Mali zao walizoacha zipo salama? Huko walipo wamepewa ulinzi?” Imehoji taarifa ya Wanamtandao hao.
Chanzo: Habarileo