Ajuza mmoja mwenye umri wa miaka 78 ambaye ni mbunge ni mtu mwenye furaha baada ya kupata digrii yake ya kwanza kutoka chuo kikuu nchini Sudan Kusini.
Kulingana na taarifa zilizochapishwa na kituo kimoja cha redio nchini humo, Victoria Adhar Arop alihitimu wiki jana na shahada ya utawala na usimamizi wa umma.
“Hii ni baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kimasomo pamoja na uzee na majukumu rasmi. Adhar ndiye mwanamke wa pili mkubwa zaidi kuhitimu katika chuo kikuu kufuatia kuhitimu kwa 2018 kwa Rebecca Agoth mwenye umri wa miaka 86 kutoka Chuo cha Sanaa na Kibinadamu,” Eye Radio waliripoti.
Akizungumza na kituo cha runinga cha SSBC, mbunge huyo ambaye pia ni mmoja wa waanzilishi wa chama cha Red Army Foundation, alisema kuwa kupitia yeye, watu wanaweza jifunza kuwa umri si kigezo cha kumzuia mtu kutofuata ndoto yake kimasomo.
“Nilijifunza na kuwaonyesha watu wengine kuwa elimu haina kikomo cha umri. Pia, kuna heshima na furaha unapoelimika. Kama sasa ninavyosalimiwa kila wakati hata katika mikusanyiko."
Adhar aliteuliwa kuwa mbunge mnamo 2005 na baadaye alichaguliwa mnamo 2010. Victoria Adhar alianza elimu yake mapema miaka ya 1950, lakini aliacha shule kutoka shule ya msingi darasa la tatu.
Baadaye alijiunga tena katika miaka ya 1970 na kuruka baadhi ya madarasa katika ngazi ya kati ili kusomea Elimu ya Juu ya Sekondari ya Sudan.