KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Watanzania watampa Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 tuzo ya heshima na iliyotukuka kutokana na kazi nzuri anayoifanya kuwaletea maendeleo.
Amesema Rais Samia ameonyesha uungwana wa hali ya juu kwa kuendelea kuchapa kazi yenye tija na kuleta matokeo mazuri ikiwamo kutekeleza miradi ya maji yenye lengo la kupunguza na kuondoa tatizo la upatikanaji wake katika maeneo mbalimbali nchini.
Shaka aliyasema hayo jana wakati akizindua mradi wa maji wa Kimbiji ulioko Kigamboni, Dar es Salaam, na kukabidhi mitambo ya kutafuta na kuchimba visima virefu vya maji pomoja na kukabidhi eneo la uchimbaji bwawa la Kidunda kwa mkandarasi atakayetekeleza mradi huo.
"Kwa heshima unayoileta, Watanzania watakupa tuzo iliyotukuka na ya heshima mwaka 2025. Mheshimiwa Rais Samia hongera sana kwa mzigo huu unaochapa,” alisema.
Yuko mshairi alisema na yuko mshairi alitunga tungo 'ada ya mja ni kunena' akimaanisha kwamba kawaida ya binadamu ni kusema 'muungwana ni vitendo' na kila aliye muungwana atatenda. Mheshimiwa Rais wewe ni muungwana wa taifa hongera sana.
"Akamalizia (mshairi) kusema tenda watu wataona majigambo weka kando. Mheshimiwa Rais unatenda, huna zogo, huna mbwembwe. Unawaletea maendeleo wananchi. Vijana wa mjini wanasema unakimbiza kimya kimya," alisema.
Shaka alisema pamoja na ukame uliopo sasa ambao umesababisha upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali, serikali inafanya kazi nzuri na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia kamati za siasa za wilaya, mikoa, sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na wajumbe wa NEC, wametembelea na kujiridhisha kuna miradi ya maji 1,194, hivyo nchi nzima inaguswa na utekelezaji huo.
