WADAU wametoa maoni kuhusu Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote pamoja na mambo mengine wakitaka kupanuliwa kwa wigo wa wategemezi hususan watoto na wenza.
Maoni hayo walitoa jana kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambapo pia walipendekeza kuwapo mfuko maalum wa kikodi ambao fedha zake zitatumika kusaidia wasio na uwezo wa kuchangia.
Mwenyekiti wa Mfuko Binafsi wa Bima ya Afya, Aaron Nelson, alisema ni muhimu kuangalia kipengele cha wategemezi kwenye muswada kuhusu idadi ya watoto na wenza ili kuondoa hali ya sasa inayolazimisha kuwa na watoto wanne na mwenzi mmoja.
Alipendekeza kitita cha msingi kishikiliwe na serikali na pale mtoa huduma anapotaka kuongeza huduma, asiwekewe ukomo.
“Sambamba na hilo, kunatakiwa kuwe na bodi huru itakayosimamia watoa huduma, serikali na watumiaji katika uendeshaji wa huduma za bima ya afya kwa wote,” alisema.
Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dk. Leons Mjwahuzi, alisema wanapendekeza kusiwapo na ukomo wa umri wa uanachama kwa wategemezi na wigo wa wanufaika uongezwe.
“Kadi za bima zipatikane kielektroniki, mchangiaji awe na uhuru wa kuchagua wategemezi na asibanwe kuweka watoto wake pekee. Pia bima ihusishe vipimo vyote, isibague vipimo vingine yaani ihusishe na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na miwani ipatikane kupitia bima ya afya,”alisema.
Chanzo: Nipashe