Wanawake waonywa, "Msikimbilie kujifungua kwa upasuaji"

WANAWAKE wanaopata ujauzito mkoani Morogoro wameshauriwa wasiogope kujifungua kwa njia ya kawaida isipokuwa inapolazimu kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro inapokea wastani wa wajawazito 600 kwa mwezi wanaopatiwa rufaa kwenye vituo vya afya katika  halmashauri za  wilaya za mkoa na kati ya hao 200 wanajifungua kwa njia ya upasuaji.

Mkuu wa idara ya magonjwa ya wanawake na uzazi wa hospitali ya rufaa hiyo, Dk Deodata Ruganuza alilieleza gazeti hili wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa huo, Fatma Mwassa.

Mwassa alifanya ziara juzi kuona shughuli za utoaji huduma za wagonjwa na miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kujengwa kupitia fedha hizo chini ya serikali ya awamu ya sita.

“Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro inazalisha wastani wa wanawake 600 kila mwezi…Na kati ya wanawake hao, 200 wanajifungua kwa njia ya upasuaji na 400 njia ya kawaida,” alisema.

Dk Ruganuza ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, alisema baadhi ya wanawake wanapenda kujifungua kwa njia ya upasuaji kutokana na kile kinachodhaniwa kuwa ni waoga wa kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Mama anayejifungua kwa njia ya kawaida anapona haraka na hapati matatizo mengi na takwimu zinaonesha wanawake waliojifungua kwa njia ya upasuaji wanaweza kukumbana na changamoto na matatizo zaidi,” alisema.

Dk Ruganuza alisema anayejifungua kwa njia ya upasuaji anaweza kukutana na tatizo la kulewa dawa za usingizi au za  ganzi, hivyo kuwa na uwezekano wa kupata matatizo yanayotokana na dawa hizo.

Alisema pia mama anaweza kupata matatizo ya kidonda kuchelewa kupona na wakati mwingne maambukuzi kwenye  kidonda.

Dk Ruganuza alisema kama hakuna sababu ya kufanyiwa upasuaji, ni bora zaidi kujifungua kwa njia ya kawaida.

Chanzo: Habarileo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo