Mzee achanjwa akidhaniwa ni mchawi wa Kijiji, aambiwa asile siku nne

Wanakijiji katika kijiji cha Seruka kilichopo wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma wamezua taharuki baada ya kujichangishana Tsh 10,000 kwa kila kaya na kuwaleta watu ambao wanaamini wangewasaidia kubaini wachawi wanaokwamisha maendeleo katika kijiji hicho ikiwemo upatikanaji wa maji.


Baadhi ya wanakijiji wanaamini kwamba matatizo wanayoyapata kijijini hapo yanatokana na imani za kishirikina 


Wananchi hao wamefanya jitihada za kumtafuta anayehusika na matatizo hayo yanayokikumba kijiji chao ikiwemo tatizo la maji ambapo baada ya kuwepo mradi wa maji kijijini hapo imeelezwa baadhi ya wazee wakiwa kilabuni walisikika wakisema "mfanye mfanyavyo maji hamuwezi kuyanywa"


Imeelezwa mkutanoni hapo kwamba idadi ya wazee 60 waliwaita wataalamu (lambalamba) wakawasafishie kisima chao cha maji (kwa maana ya kutambika), ambapo walichangishana mchango wa shilingi 10,000 kila kaya kwa ajili ya kuwaleta hao wataalamu wa kuwabaini wachawi wa maendeleo katika kijiji chao ikiwemo waliozuia upatikanaji wa maji


Tambiko lililofanywa kwenye kisima cha maji halikuzaa matunda ambapo Oktoba 18,2022 operesheni hiyo ilimkumba Mzee Zabblon Malole ambaye amesema mbele ya mkutano wa kijiji hicho na mkuu wa wilaya ya Mpwapwa Josephat Maganga kwa kusimulia machungu yake aliyopitia, ikiwemo jinsi alivyokamatwa na watu hao maarufu kama lambalamba akachanjwa chale, na kupewa masharti ya kutokula Ugali (Chakula) kwa siku 4 mfululizo, wakati wakisubiri majibu ya "ndumba" hiyo aliyofanyiwa


Mkuu wa wilaya Josephat Maganga ameshangazwa na maelezo ya Mzee huyo na Kumuagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) kwenda na Mzee huyo hadi nyumbani kwake asimamie akipikiwa chakula na kukila, na endapo chochote kitampata lambalamba na watu wote waliohusika  watakiona cha mtema kuni


Amewataka watoto wake waliokuwepo kwenye mkutano huowakampikie baba yao chakula, ale na akatoe maelezo yake polisi ndipo hatua zianze kuchukuliwa huku akimtoa hofu na wasiwasi Mzee huyo kuhusu usalama wa maisha yake


Pia Mkuu wa wilaya ameagiza Mzee huyo apelekwe hospitali akachunguzwe kama kupitia chale alizochanjwa amewekewa sumu, "apimwe damu yake tuone kama amewekewa sumu, majibu yale yatatusababisha sisi tuchukue hatua za kisheria dhidi ya yeyote aliyeshiriki katika tendo hilo".




JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo