Muuguzi wa magonjwa ya akili Mkenya anayefanya kazi Marekani aliuawa kwa kudungwa kisu na mgonjwa wake alipokuwa akimhudumia.
June Onkundi alikuwa akimhudumia James Gomes ambaye ana historia ndefu ya ugonjwa wa akili lakini hakunusurika Jumanne iliyopita.
Mwanamume ambaye alikuwa akijaribu kuokoa maisha yake, badala yake alichukua yake.
Familia ya mama huyo wa watoto wanne na mke inamtaja kama mwanamke mwenye huruma ambaye alipenda jamii ya eneo lake na alijitolea yote katika kutunza afya zao.
Walichukua maisha yake kama malipo, alisema Andrew Nyabwari, kakake Onkundi.
"Watu walewale ambao alikuwa na shauku na hamu ya kusaidia ndio ambao hatimaye walimchukua kutoka kwetu na kutuacha tukiwa na majonzi na watoto wanne na mume," Nyabwari aliambia ABC NEWS 11 yenye makao yake Raleigh, North Carolina.
Onditi Nunda, binamu ya Onkundi anayeishi Texas, aliambia kituo hicho kwamba muuguzi huyo aliithamini sana familia yake na kwamba angejitolea kwa ajili yao bila kufikiria.
"Alikuwa mtu ambaye anathamini sana familia. Kila kitu ambacho angefanya ni cha familia. Hicho ndicho nitakachomkumbuka," alisema Nunda.
Muuguzi huyo wa magonjwa ya akili alifanya kazi katika Kituo cha Urejeshaji cha Freedom House katika kaunti ya Durham, North Carolina, ambapo alikuwa na shauku ya kusaidia wagonjwa wa akili, na alikuwa na sifa ya kufanya kazi kama daktari msaidizi kusimamia matibabu na kutoa maagizo.
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, Mmarekani mweusi mwenye umri wa miaka 47 Gomes ni mhalifu wa mfululizo ambaye ana tabia ya kuwalenga wahudumu wa afya wanaomhudumia au wafanyakazi wenzake.
Pia ametumia karibu nusu ya maisha yake gerezani baada ya kukutwa na hatia ya uhalifu.