Mshtakiwa aeleza sababu za kumuua mkewe, Aachiwa kisha akamatwa

MFANYABIASHARA Khamis Luwonga (38), anayedaiwa kumuua mkewe, Naomi Marijani, kwa kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, ameeleza sababu za kutekeleza kitendo hicho.

Luwonga alitaja sababu hizo baada ya kuachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kueleza kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yake. Hata hivyo, baadaye alikamatwa tena na kusomewa upya mashtaka.

 

Mshtakiwa huyo alidai kuwa mke wake kila siku alikuwa anamwomba Mungu afe kuliko kuendelea kuishi katika ndoa yao na alikuwa anang'ang'ania kifo chake kwa nguvu. Kutokana na kifo hicho, kwa sasa mtoto wao anaishi bila wazazi.

 

Pia alidai kifo cha mke wake hakikusababishwa na yeye peke yake bali wengine waliohusika ni familia za pande zote za mbili, maofisa wa polisi na watumishi wa ngazi za chini za serikali.

 

Luwonga alizungumza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga, baada ya hakimu huyo kumaliza kutoa uamuzi wa kumwachia huru mshtakiwa kama upande wa Jamhuri ulivyoomba chini ya kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

 

Mshtakiwa alianza kwa kuomba radhi kwa hakimu kwa kutaka kujua jina lake ili ajue anazungumza na nani kwa sababu amesahau jina lake, lakini Ruboroga alimweleza kwamba yeye aendelee kusema anachokitaka.

Ilipofika saa 8:26 mchana, mshitakiwa alipandishwa tena kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Rhoda Ngimilanga wa mahakamani hiyo na kusomewa upya mashtaka ya mauaji.

 

Wakili Ally alidai upelelezi haujakamilika na kuomba wapangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa, Ngimilanga aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 7, 2022.

 

Mshtakiwa amerudishwa mahabusu hadi tarehe hiyo kwa sababu kisheria shtaka la mauaji halina dhamana na pia hakutakiwa kujibu kweli au si kweli kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza shauri lake.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo