Watoto wateketea kwa moto mama akilewa chakari kilabuni

Watoto wawili wamefariki dunia baada ya nyumba yao kuteketea kwa moto katika Mtaa wa Mafifi, Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa huku mama yao akiwa analewa kilabuni.


Kwa mujibu wa mashahidi wa tukio hilo, watoto hao, Rehema Masanga (7) na Amos Masanga (5) walishindwa kujiokoa baada ya mama yao, Skolastica Mgombewa kufunga mlango kwa nje akiwaacha peke yao na kwenda kilabuni kunywa pombe.

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mafifi, Rabi Mgata, aliiambia Nipashe kuwa chanzo cha moto huo ni mshumaa ambao ulishika godoro kisha kuunguza nyumba yote.

 

“Mama yao aliwafungia watoto ndani akaenda kunywa pombe. Kwa hiyo moto ulivyokuwa unaendelea kuwaka walishindwa kujiokoa. Mama alirudi baadaye akiwa amelewa wakati tayari tumeshazima moto na kugundua watoto wamekufa,” alisema.

 

Mgata alisema taarifa za nyumba hiyo alizipata jana saa 4:00 usiku na kwenda  kwenye tukio ambako tayari watu walikuwa wameanza kuzima moto.

 

Alisema baada ya kuzima moto, walibomoa mlango na kukuta watoto wawili waliokufa huku wakiwa wamekumbatiana kwenye kona moja ya nyumba.

 

Baadhi ya majirani walisema awali walianza kuona moshi ukifuka lakini wengine walidhani ni wa matairi.

 

Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Iringa, Isabela Bwago, amekiri kuwa chanzo cha tukio hilo ni mshumaa ambao ulishika godoro kisha kuunguza nyumba yote bila kuokoa kitu chochote.

 

“Ni uzembe wa mzazi ambaye aliondoka akiwa amewafungia watoto wake kwa nje. Taarifa ya moto tulipewa kwa kuchelewa na hata ingekuja mapema gari lisingeweza kufika eneo la tukio kulingana na miundombinu mibovu,” alisema Bwango.

 

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Issa Juma, alisema wakati jamii inahangaika kuzima moto huo hawakujua kama ndani kuna watoto.

 

Juma aliitaka jamii kuwa makini na matumizi ya mishumaa, vibatari, taa na kuwa walinzi wa familia zao hasa watoto.

 

“Niwasihi wazazi na walezi kuwa makini na waweke uangalizi kwa watoto kwa kuchukua tahadhari ili kuepuka vifo vinavyoweza kuzuilika,” alisema.

Imeandikwa na Martha Sambo kupitia Gazeti la Nipashe.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo