Picha: Mgombea wa CHADEMA Aliyetekwa aonekana akiwa Hoi

Mgombea wa udiwani Kata ya Buhangaza, Muleba (Chadema), Athanasio Makoti aliyekuwa amepotea tangu Februari 2, mwaka huu amepatikana. CHADEMA imesema alitupwa barabarani maeneo ya Hospitali ya Kagondo.

Chadema.jpg
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU KUTEKWA KWA MGOMBEA WA UDIWANI BUHANGAZA (CHADEMA), NELSON ATHANAS MAKOTI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa tahadhari kubwa tukio la kutoweka katika mazingira yenye utata kukiwa na viashiria vya utekwaji kwa Mgombea wa Udiwani Uchaguzi Mdogo wa Kata ya Buhangaza, Muleba, Ndugu Nelson Athanas Makoti, huku Jeshi la Polisi wilayani humo likisuasua kufungua jalada la uchunguzi wa tukio hilo kwa siku mbili, hadi alipoonekana usiku wa kuamkia leo akiwa taaban na hajiwezi.

Kutokana na mwenendo uliooneshwa na polisi Wilaya ya Muleba katika tuko hilo na kauli iliyotolewa na polisi ngazi ya mkoa, tunatoa wito kwa jeshi hilo Makao Makuu kuingilia kati ili uchunguzi wa haraka kuhusu suala hilo ufanyike kwa ajili ya haki kutendeka na hatua za kisheria kuchukuliwa.

Mbali ya Jeshi la Polisi Makao Makuu, pia tunatoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBU) kutumia mamlaka yake ya kikatiba na kisheria kuhakikisha tukio hilo linafanyiwa uchunguzi wa haraka na kina kuwabaini wahusika na kuchukua hatua.

Aidha, Chama kinaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoka hadharani kukemea vitendo kama hivyo ambavyo vinatia doa mfumo wa uchaguzi na demokrasia nchini. Ukimya wa Tume ya Uchaguzi unaashiria kuwa wanakubaliana na tabia hii mpya ya utekaji ambayo tuliilalamikia hata wakati wa uchaguzi wa marudio wa Kata 43 ambao ulipelekea baadhi ya Vyama vya Upinzani kususia uchaguzi wa

marudio uliofanyika Januari 13, vikiwa na lengo la kuwaambia Watanzania na dunia nzima kuhusu ukiukwaji wa misingi ya uchaguzi, zikiwemo sheria, kanuni, maadili na miongozo mbalimbali.

Halikadhalika, tunaomba makundi mbalimbali katika jamii, hususan taasisi za masuala ya utetezi wa haki za binadamu na vyama vya siasa kuendelea kuunganisha nguvu, kulaani na kupinga vikali matukio ya namna hii katika jamii yetu.

Chama kimefikia hatua hiyo baada ya kufuatilia kwa karibu taarifa za tukio hilo tangu habari za kutoweka kwa Ndugu Makoti zilivyopatikana.


Awali tukio hilo lililotokea Februari 2, mwaka huu majira ya jioni, wakati Makoti akiwa njiani kurudi nyumbani kwake, liliripotiwa polisi, kituo kidogo cha Polisi Ijumbi kisha baadae Polisi Muleba mjini.


Jambo la kushangaza ni kwamba, tangu siku ya Jumamosi, Februari 3, mwaka huu, taarifa hizo zilipofikishwa kwa polisi Muleba na viongozi wa CHADEMA wilayani humo, pamoja kufanya kikao na viongozi wa chama na familia ya Makoti, jeshi hilo halikufungua jalada la kesi wala hawakutoa namba ya RB kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo kama taratibu za kisheria zinavyoelekeza, kwa sababu ambazo hazieleweki.


Viongozi wetu waliporejea kituoni hapo siku iliyofuata, Jumapili Februari 4, kufuatilia hatua zilizofikiwa, waliambiwa kuwa jalada halijafunguliwa wala wasingeweza kupata RB Namba kwa sababu anayehusika na majukumu hayo hakuwepo ofisini. Kwa hiyo hakukuwa na uchunguzi wowote uliokuwa unaendelea kwa tukio zito kama hilo.


Katika mtiririko huo huo unaoweza kuhojiwa na kutiliwa shaka, jioni ya Februari 4, Kaimu RPC wa Mkoa wa Kagera, Isack Msangi alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akitoa masharti kwa wananchi ambao wanaweza kuwa na taarifa za kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.


Aliwaambia wananchi wasitoe taarifa za kuegemea upande mmoja wa kisiasa na kuutuhumu mwingine. Jambo hilo si sahihi hata kidogo. Tunaamini kazi ya wachunguzi wa polisi ni kupokea taarifa na kuzifanyia kazi, ikiwemo kuchuja sio kuelekeza zitoleweje na kwa mtizamo gani! Maelekezo hayo ya polisi yanaweza kuwatisha wale wote wanaoweza kusaidia taarifa zenye ushahidi wa tukio hilo.


Aidha yanaweza kuepusha wahusika kujulikana na pengine jeshi hilo kushindwa kupata viashiria vinavyoweza kusaidia kubaini mtandao wa watu 'wasiojulikana' ambao wamekuwa wakidaiwa kupoteza au kuteka watu katika matukio mengine yanayofanana na hilo la Makoti.


Baada ya Ndugu Makoti kuonekana usiku wa kuamkia leo baada ya kutupwa barabarani kisha kusaidiwa kufika Hospitali ya Kagondo akiwa hoi kwa maumivu makali, akilalamika kupigwa sana na watu waliomteka, wakiwa wamejifunika vitambaa usoni, tunasisitiza tena;


Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola vitimize wajibu wake katika tukio hilo la kutoweka kwa Ndugu Makoti, huku vikitambua kuwa CHADEMA mbali ya kulaani vikali tukio hilo, kinasikitishwa na hakiridhiki na hatua na kauli zilizochukuliwa au kutolewa na jeshi hilo wilayani Muleba na mkoani Kagera, hasa ikizingatiwa kuwa tukio la Ndugu Makoti ambalo limetokea katikati ya kampeni za uchaguzi mdogo, limetukumbusha matukio ya kukamatwa kwa wanachama na viongozi wetu na kushikiliwa na polisi Muleba kinyume cha sheria, lakini pia kushambuliwa kwa risasi na watu wa CCM bila hatua yoyote kuchukuliwa wakati wa uchaguzi mwingine wa marudio, Kata ya Kamwani, uliofanyika Januari, mwaka jana. Ni muhimu pia polisi wakajibu swali linaloanza kujitokeza kuna nini huko Jimbo la Muleba Kusini, linaloongozwa na mmoja wa makada maarufu wa CCM mkoani Kagera, Prof. Anna Tibaijuka.


Vyombo vya dola vijikite kuhakikisha, wahusika wa tukio la Ndugu Makoti wanajulikana na kuchukuliwa hatua stahiki ili kukomesha matukio ya namna hiyo yanaoonekana kushamiri nchini.


Ni muhimu sana vyombo vya dola vikaonesha mwenendo ambao utawashawishi wananchi waamini kuwa kweli vinachukizwa na


vitendo vya upoteaji, utekwaji na kushambuliwa kwa risasi kama matukio hatarishi sana ya usalama wa raia na mali zao.


Mojawapo ya dalili za mwenendo sahihi ni kuchukua hatua za haraka za uchunguzi wa matukio ya namna hiyo na kutoa taarifa. Kinyume na hayo, vyombo hivyo vitakuwa vinahalalisha vyenyewe kuendelea kuwekwa katikati ya shutuma na tuhuma kila matukio ya namna hiyo yanapojitokeza.

Imetolewa leo Jumatatu Februari 5, 2018 na;

Tumaini Makene

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano CHADEMA


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo