Naibu waziri wa madini Stanslaus Nyongo amewataka wamiliki wa mgodi wa GGM, mkoani Geita kuwalipa fidia wananchi ambao wamewaondoa kwenye maeneo yao na kuacha visingizio vinavyowakandamiza wananchi
''Unakuta mtu kazaliwa hapo kakulia hapo amejenga ana watoto halafu mtu anakuondoa kwa madai kuwa upo kwenye leseni yake hainiingii akilini, kama unahitaji eneo langu njoo tukae tumalizane unipe changu mimi nisepe inakuwa nilipe nisepe ” amesema Nyongo.
Nyongo ametoa kauli hiyo wakati akiongea na wananchi wa kijiji cha Nyakabale kata ya Mgusu, Wilayani Geita kwenye ziara yake ya siku mbili Mkoani humo, ya kuzungukia maeneo ya uchimbaji pamoja na kusikiliza kero za wananchi ambao wanazunguka kwenye baadhi ya maeneo ya mgodi wa Geita(GGM).
Hatua hiyo ya Naibu waziri Nyongo imekuja baada ya kusikia malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya mgodi wa GGM kushindwa kuwalipa fidia kwa muda mrefu wananchi ambao wanaudai mgodi huo kutokana na kuwaondoa kwenye maeneo yao.
Hata hivyo amewataka wamiliki wa mgodi huo kuwalipa wananchi hao ama waondoke wawaachie eneo lao waendelee kuchimba, kwani mgodi ulikuja kama neema hivyo hautakiwi kugeuka kuwa kitu cha kunyanyasa wananchi.