Watoto wawili wa kike walioungana wamezaliwa katika Kituo cha afya Omukajunguti wilayani Missenyi mkoani Kagera.
Watoto hao wenye afya njema wamezaliwa kwa upasuaji leo Jumatatu Januari 29,2018 wakiwa wameungana kuanzia kifuani na wana miguu mitatu.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, mtawa Dk Fransisca Francis amesema afya ya watoto hao na mama yao, Jonesia Jovitus ni nzuri.
“Tulimpokea mama huyu akiwa na uchungu wa kujifungua saa nane usiku wa kuamkia leo Januari 29,2018, tulimfanyia upasuaji na alijifungua salama,” amesema Dk Fransisca.
Amesema, “Jonesia alikuwa na uzazi pingamizi na asingeweza kujifungua kwa njia ya kawaida.”
Akizungumza hospitalini hapo, Jonesia ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyankere kata ya Mabale wilayani Missenyi amewaomba wasamaria wema kujitokeza kumsaidia gharama ya chakula na matunzo kwa watoto wake.
“Kwa jinsi walivyo najua watoto wangu watahitaji huduma maalumu ya afya, chakula, mavazi na malazi; huo ndiyo msaada ninaoomba kwa wasamaria wema,” amesema Jonesia.
