Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma imesema Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis atafikishwa mahakamani kesho.
Kamanda wa Takukuru mkoani Dodoma, Emma Kuhanga amesema Sadifa atafikishwa mahakamani kesho Jumatatu Desemba 11,2017.
Amesema kiongozi huyo alikamatwa nyumbani kwake akiwapa soda wajumbe wa UVCCM kutoka Mkoa wa Kagera kitendo ambacho ni kinyume cha maadili.
UVCCM leo Jumapili Desemba 10,2017 inachagua viongozi wapya wa ngazi ya Taifa watakaoongoza jumuiya hiyo ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano.
Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge, Zanzibar amekamatwa nyumbani kwake Mailimbili mjini Dodoma.
Awali, Kuhanga akithibitisha kukamatwa kwa mwenyekiti huyo alisema, “Ni kweli tumemkamata tangu jana usiku tumekesha tunafanya uchunguzi, nitatoa taarifa baadaye kuhusu tukio hilo," amesema.
Chanzo:mwananchi
