Mamlaka nchini Tanzania imezuia uzinduzi wa ripoti kuhusu unyanyasaji wa wafanyikazi wanawake kutoka taifa hilo wanaofanya kazi katika mataifa ya Uarabuni.
Shirika la Human Wrights Watch limedai katika matokeo yake kwamba wafanyikazi wa nyumbani kutoka nchini Tanzania walikuwa wakibakwa , kuteswa na kulipwa mishahara duni na waajiri wao katika mataifa ya Uarabuni.
Ripoti yenye kurasa 100 inayodai kuteswa kwa wafanyikazi wa nyumbani wa Tanzania nchini Oman na muungano wa mataifa ya Emirata UAE ilitarajiwa kutolewa leo kwa waandishi wa habari mbele ya waathiriwa lakini hilo halikufanyika.
Katika hatua isiokuwa ya kawaida ,afisa mmoja kutoka shirika linalofadhiliwa na serikali la Sayansi na Teknolojia COSTEC William Kindekete alifutilia mbali mkutano huo katika mji mkuu wa Dar es Salaam akisema kuwa wanaharakati wa shirika hilo la haki za kibinaadamu hawakufuata sheria katika kufanya utafiti wao.
Hatahivyo matokeo ya utafiti huo wa HRW unaonyesha kuwa takriban wanawake 50 walihojiwa wakati wa utafiti huo ambao wanadai kwamba walilazimishwa kufanya kazi kwa kati ya saa 15 na 21 kwa siku huku wakipokonywa pasipoti zao na waajiri wao punde tu walipowasili katika mataifa hayo.
Ripoti hiyo ilibaini zaidi kwamba zaidi ya nusu yao hawakulipwa huku wengine wakisema kuwa hawakulipwa kabisa.
Wawili kati ya watano walidai kupigwa mbali na kunyanyaswa kijinsia.
Ripoti hiyo ya HRW pia inasema kwamba balozi za Tanzania katika eneo la Ghuba hazikutoa usaidizi wowote kwa waathiriwa wakati walipotaka usaidizi .
Juhudi za kupata majibu kutoka kwa serikali ya Tanzania hazikufanikiwa kwa kuwa maafisa wengi hawakuwa tayari kuzungumzia swala hilo.
Chanzo: bbc