Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema iwapo Sheria Namba Tano ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 itawasilishwa bungeni wa ajili ya kupitishwa watakuwa tayari kufa kuliko kukubali ipitishwe.
Akizungumza jana Jumanne jioni wakati wa kumnadi Mgombea Udiwani wa Kata ya Ibhigi, iliyopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Emmanuel Simba, Mbowe amesema kama kuna wakati wanaume wanatakiwa kusimama wahesabiwe ni wakati huo.
Alisema kupitisha sheria hiyo maana yake ni kuingiza ubatili walioufanya ili uwe sheria kamili, kwamba hakuna mikutano ya vyama vya siasa, hakuna majadiliano ya mustakabali wa nchi.
"Wanaanda mkakati wa kubadilisha sheria ya vyama vya siasa taarifa tunayo, wanataka kuiingiza sheria hiyo kwa nguvu, Sugu(Joseph Mbilinyi) tunaanzia bungeni, wakati huo ukifika wakituua watuue, wakitunyonga watunyonge hatutakubali tutaandamana mahali popote," alisema Mbowe.
Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai alisema watalikataa hilo ili watoto watakaokuja kesho na keshokutwa wajue baba na mama zao walipambana kulipigania Taifa lao.
Alisema Watanzania kwa umoja wao wasilikubali hilo kwa sababu litawanyima haki kukutana na kujadili wanataka nini kifanyike na watakuwa wamekubali kurudi nyuma miaka mitano.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyokutana juu na wawakilishi wa vyama vya siasa , ambapo ilitoa tamko kuwa katika kampeni za uchaguzi wa marudio ya udiwani, wasijadili masuala ya siasa nje ya kata, jambo ambalo ni la kipuuzi.
Alisema "tusipokuwa makini na haya matamko ipo siku tutaambiwa wake zetu walale upande huu na sisi upande huu”
"Wanataka mimi mwenyekiti wa chama Taifa nije kujadili masuala ya kata, halafu masuala ya Taifa atajadili nani," alihoji Mbowe.
Alisema wamezuiliwa kuzungumza na wananchi kwa miaka miwili sasa ndiyo nafasi pekee waliyopata kuzungumza nao, "Haya ni makatazo ya kipuuzi," alisema.
Mbowe pia alizungumzia kashfa zinazodaiwa kufanywa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema kama wana uhakika na tuhuma hizo wampeleke mahakamani.
"Ilianza kwa Edward Lowassa alipohamia Chadema, ikaja kwa Fredrick Sumaye na sasa Nyalandu, kila anayehamia upinzani anaitwa fisadi, sisi hatuogopi Mahakama kwa sababu tunajiamini, wawachunguze na wawapeleke mahakamani.
" Nimezungumza na Nyalandu asubuhi ya leo, nikamuuliza kuhusu tuhuma hizo atachomoa, akasema hilo ni jambo dogo atadili nalo na halimpi shida," alisema Mbowe.