Lazaro Nyalandu amesema hayo leo kupitia mitandao yake ya kijamii na kusema wabunge mbalimbali wamekuwa wakimuunga mkono kuhusu hoja ya kutaka kurejeshwa upya mchakato wa Katiba Mpya ambapo amepanga kuwasilisha bungeni katika Bunge la tisa linalotegemewa kuanza Novemba 7 mwaka huu mjini Dodoma.
"Nawashukuru wabunge wenzangu CCM na Upinzani wanaounga mkono hoja ya kurejea upya rasimu ya Katiba Mpya kama iliyopendekezwa na Tume ya Warioba" alisema Nyalandu
Mbali na hilo Mbunge huyo amezidi kuwaomba Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokubali hoja zitakazopelekwa Bungeni zikiwa na lengo la kutaka kukiuka ukomo wa uongozi uliowekwa na Katiba wa miaka mitano na kuwataka Wabunge hao kujikta zaidi katika kupata Katiba Mpya ya Tanzania.
Hivi karibuni Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia alisema anakusudia kupeleka hoja Bungeni ili kufanya marekebisho ya Katiba na kuongeza ukomo wa uongozi kutoka miaka 5 mpaka miaka 7 kwa kila awamu. Jambo ambalo Nyalandu analipinga.