Jana nilikuwa nasoma gazeti moja, katika ukurasa wa mbele wameandika “Asilimia 67 ya Watanzania wanatumia ARVs,” nilipo liona nikajua wamekosea bahati mbaya nikaamua kufungua ndani nione kama walirekebisha.
Nilipofungua ndani, nilikuta kichwa cha habari kile kile, nikasema ngoja nisome, labda watakuwa wamerekebisha humu ndani, lakini habari ikawa vile vle kuwa watanzania 67% wanatumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI.
Hayo yamesemwa leo na Rais Magufuli alipokuwa anatoa wito wake kwa waandishi wa habari nchini kuwa wazalendo na kuandika habari za kujenga kwani akiandika habari za kupotosha, wanaichafua Tanzania.
Rais alisema hayo kwenye hafla ya kutoa vyeti kwa wajumbe wa kamati mbalimbali zilizohusika katika mchakato mzima wa madini, na kufanikisha kufikiwa kwa makubaliano ambayo yameweka mwanzo mzuri wa serikali kuanza kunufaika na rasilimali zake.
Rais alisema baada ya kusoma hiyo habari alishtuka, na kuamua kumpigia simu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ili apate ufafanuzi, na ndipo waziri akasema taarifa hiyo si ya kweli.
Waziri Mwalimu alisema kuwa, alichokisema wakati wa Tsh 860 milioni kwa ajili ya kununua dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI ni kwamba, jumla ya watanzania milioni 1.4 wameathirika na virusi vya UKIMWI na kwamba miongoni mwao (walioathirika), ni asilimia 67% pekee wanaotumia ARVs na kwamba lengo la serikali ni kufika asilimia 90% ifikapo mwaka 2020.
Taarifa hiyo iliandikwa kwatika gazeti la kila siku la TanzaniaDaima ambalo hutolewa na Kampuni ya Free Media inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe.
Rais Magufuli alisema kwamba, taarifa kama hiyo inapoandikwa, inamadhara makubwa kwa nchi kwani hata wawekezaji hawawezi kuja kwenye nchi ambayo inaelezwa asilimia 67 ya watu wake wameathirika na UKIMWI kwa sababu anajua hata akija hatopata nguvu kazi ya kutosha kufanyakazi kwenye kiwanda/kampuni yake.
Lakini pia alisema, taarifa hiyo inaweza kutishia hata watalii waliopanga kuja kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii vilivyopo nchini Tanzania.