Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewahakikishia wazazi, walezi, wanafunzi na wadau wa elimu Mkoani hapa kuwa Singida haitapata ufaulu mbaya kielimu kama ilivyokuwa mwaka huu kutokana na mikakati iliyowekwa.
Dkt Nchimbi ametoa hakikisho hilo mapema jana ofisini kwake alipokutana na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha wadau wa elimu kilichoweka mikakati ya kuinua ufaulu wa kielimu mkoani hapa.
Dkt Nchimbi amesema baada ya Mkoa wa Singida kufanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba yaliyotoka hivi karibuni, wadau muhimu walikutana kutafakari changamoto na suluhisho ili ufaulu uwe mzuri katika mitihani ijayo.
"Mwaka jana tulikuwa wa 12 kati ya mikoa 26 tukiwa na ufaulu wa asilimia 69 lakini mwaka huu tumekuwa wa 26 na ufaulu umeshuka hadi asilimia 61, ufaulu huu haumfurahishi mtu yoyote yule", amesema na kuongeza kuwa,
"Kama Mkoa tumejua sehemu tulipokosea hivyo tumeweka mikakati, kwanza tutahakikishwa wanafunzi wa shule zote za Msingi wanapata chakula shuleni, pili walimu wote watapewa motisha ya viwanja kwa utaratibu ulio rafiki na mishahara yao, tatu tumeipatia Tume ya Utumishi wa Waalimu (TSC) miezi mitatu iweze kusikiliza kesi na malalamiko ya waalimu", amefafanua Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa Mkoa utaongeza ukaguzi pamoja na kuwakutanisha wathibiti ubora na maafisa elimu ili waweze kushirikiana vizuri katika kuhakikisha elimu bora inatolewa mashuleni.
Dkt Nchimbi ameeleza kuwa baadhi ya changamoto ambazo zimeonekana kuwa kikwazo kikubwa katika kuinua ubora wa elimu ni pamaoja na kutokuwa na usimamizi na ukaguzi wa karibu wa elimu Singida huku waalimu wakiachiwa jukumu la kusimamia elimu bila kukaguliwa mara kwa mara.
Ameongeza kuwa waalimu wamekuwa na malalamiko mbalimbali lakini maafisa utumishi wameshindwa kuwasaidia hivyo kuwakatisha tamaa huku akiwataka waalimu kufundisha mada zote na zile wanazopata ugumu kutakuwa na utaratibu wa walimu 'tembezi' kutoka shule nyingine watakaowasaidia kwa kipindi hiki.
Aidha Dkt Nchimbi ameishukuru serikali kuleta mkakati wa kuboresha elimu 'EQUIP' utakaodumu kwa muda wa miaka miwili kwakuwa utasaidia kutatua baadhi ya changamoto za elimu Mkoani hapa.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Singid Florian Kimolo amesema amesikitishwa na hali ya ufaulu kwa matokeo ya darasa la saba mwaka huu na kueleza kuwa hali hiyo haipendezi na haikubaliki.
Kimolo amesema idara yake itaimarisha ufatiliaji pamoja na kufanyia kazi taarifa za ukaguzi kutoka kwa wadhibiti ubora wa elimu pamoja na kusimamia ufanisi wa wanafunzi katika kuzijua K. K. K tatu ambazo ni kusoma, kuhesabu na kuandika.
Ameongeza kuwa jitihada nyingine zitawekwa katika kuwaelimisha wazazi/walezi waweze kuwasimamia watoto wao katika masomo pamoja na kuwahamasisha kupenda elimu .