Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Tandika jijini Dar es Salaam na Abajalo kutoka Sinza maarufu kama Mnyama ikapoteza kwa mabao 3-0. Baada ya kipigo hicho, Mahadhi aliangua kilio akisema wachezaji hawakuonyesha juhudi na wakati mwingine alionekana kutofurahishwa na maamuzi.
Baadhi ya watu wa Ajabalo walilazimika kumtoa eneo hilo la uwanja na kumuingiza vyumbani huku akiendelea kulia. Lakini baadaye ilielezwa, hali yake ilizidi kuwa mbaya baada ya presha kupanda, akaanguka juhudi zilifanyika kumkimbiza hospitali, lakini baadaye alifariki dunia.
Mahadhi alikuwa akimsaidia Kocha Abdallah Kibadeni ambaye kila alipopata nafasi alikwenda kutoa ujuzi wake kwa timu hiyo ya mtaani kwao. Abajalo ni timu ya mtaani kwa Kibadeni na Mahadhi ambao walikuwa wanaishi nyumba jirani Sinza kabla ya kuhama.
Mahadhi ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa soka, pia ni kaka wa kiungo wa zamani wa Yanga, Waziri Mahadhi 'Mendieta'.
Kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, amesema msiba wa Rashid aliyewika miaka ya 1990 katika Ligi Kuu ya Bara, upo nyumbani kwake, Kimara Bonyokwa na mwili wa marehemu utasafirishwa mapema kesho kwa mazishi kwenye makaburi ya Mnyangani, Tanga.
Waziri amesema marehemu ambaye alipatwa na ugonjwa wa kiharusi kwa zaidi ya mwaka sasa, ameacha mke, Jazira na mtoto, Mahadhi mwenye umri wa miaka 18 sasa. Mungu aipumzishe kwa amani roho ya marehemu. Amina