Hii Ni Picha ya Yule Mtekaji watoto huku akidai fedha

Polisi mkoani Geita kwa kushirikiana na polisi wa Mkoa wa Arusha wamemtia mbaroni mtuhumiwa wa utekaji watoto akiwa na mtoto mwenye umri wa miaka miwili katika nyumba ya kulala wageni ya Shitungulu, Katoro Wilaya na Mkoa wa Geita aliyekuwa akimshikilia akidai apewe Sh milioni nne.
Samson Peter amekamatwa usiku wa kuamkia jana baada ya timu maalumu ya Polisi ya askari tisa, watano kutoka Arusha wakiongozwa na Mkaguzi wa Polisi Amani na askari wanne wa Geita wakiongozwa na Mkaguzi wa Polisi, James, kuizingira nyumba ya wageni aliyokuwa amejificha mtuhumiwa na mtoto aliyemteka tangu Septemba Mosi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema mtuhumiwa alikamatwa saa mbili usiku juzi katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Shitungulu katika Mtaa wa California, Kata ya Katoro wilayani Geita akiwa chumba namba 11 na mtoto huyo Justine Ombeni miaka miwili aliyemteka, akiwa hai na afya njema.
Kamanda Mwabulambo alisema mtoto huyo alitekwa Septemba Mosi saa nane mchana wakati akicheza na watoto wengine watatu mbele ya nyumba yao baada ya mtuhumiwa kufika na kuwagawia jojo watoto wengine watatu na kisha huyo wa nne akamchukua.
Alieleza kuwa baada ya kuwalaghai watoto wengine, aliondoka na mtoto huyo na kutokomea kusikojulikana hadi wazazi walipotoa taarifa Kituo cha Polisi Geita na wakati baba wa mtoto huyo anarudi nyumbani kutoka kuripoti Polisi zikiwa zimepita saa nne baada ya utekaji, alikuta ujumbe wa karatasi unaoonesha namba ya simu ya mtekaji ukielekeza awasiliane naye kwa simu hiyo.
Ujumbe huo alipatiwa kijana mwenye umri wa miaka 13 wa jirani ambaye bila kufahamu una lengo gani aliufikisha nyumbani kwa familia na ndipo ufuatiliaji ulipoanza wa mtoto kwa kuwasiliana kupitia simu hiyo ambayo katika mawasiliano, mtekaji alitoa masharti ya kutumiwa Sh milioni nne kupitia mtandao wa M-Pesa.
Wakati mtekaji huyo akitekeleza ukatili huo, wakati huohuo alikuwa akisakwa mkoani Arusha kwa tuhuma za kuteka watoto wanne na kisha kujipatia Sh 300,000 kwa njia hiyo ya kupitia mtandao wa simu na kuwaachia watoto wawili kati ya wanne anaodaiwa kuwateka.
Watoto wawili kati ya hao wanne hawajulikani waliko. Kwa mujibu wa taarifa za kipolisi, imedaiwa kuwa baada ya kutenda ukatili huo mkoani Arusha kati ya Juni na Agosti, mtuhumiwa alitoroka na kurudi mkoani Geita na kuendeleza ukatili huo hadi alipotiwa mbaroni na timu hiyo ya askari polisi waliokuwa wakitumia weledi na utaalamu wa ufuatiliaji mitandao ya simu.
Mama mzazi wa mtoto aliyetekwa, Elizabeth Ombeni  na Baba wa mtoto huyo, Ombeni Mshana kwa pamoja wanaishukuru serikali na Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri waliyoifanya ni mfano wa maadili mema na kujituma kwa dhati katika ufuatiliaji na kupambana na uhalifu.
“aliyemteka mwanangu alinionya nisithubutu kushirikiana na polisi kumsaka nikifanya hivyo atamkata mikono na miguu mtoto wangu hivyo nikaogopa na nikataka kutuma kiasi cha fedha ili amwachilie mwanagu” alisema baba mzazi wa mtoto.
Hata hivyo, alisema polisi walimzuia na kumtia moyo asitume fedha, na hadi mtuhumiwa anakamatwa alikuwa hajampatia fedha kiasi chochote.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Samson Peter amekiri kuhusika na kuwa amekuwa akisukumwa na tamaa kupata fedha za matumizi kwa maisha ya anasa baada ya kukatisha masomo akiwa kidato cha tatu na alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kilimani katika Kata ya Katoro.
Akizungumza na wanahabari baada ya kukamatwa, Peter amekiri kumteka mtoto Justine ili ajipatie fedha jaribio alilokiri kugonga mwamba na kuwa kati miezi miwili iliyopita, akiwa jijini Arusha pia aliteka watoto wanne akiwemo msichana mmoja na kupata Sh 300,000 kabla ya kurudi mkoani Geita.
Hata hivyo, baada ya wazazi wa watoto wengine wawili kushindwa kumpatia fedha kupitia mtandao, aliwatelekeza na kuondoka huku wengine wawili akiwarudisha maeneo aliokuwa amewateka ili warudi kwa wazazi wao kwa kuwaachia huru baada ya kumpatia fedha hizo kupitia mtandao wa simu.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo