Na Rhoda Ezekiel
MKUU wa wilaya Buhigwe mkoa Kigoma, Kanali Marco Gaguti ameendesha zoezi la kustukiza la ukaguzi wa hali ya ulinzi na usalama wa mpaka wa Tanzania na Burundi na kuridhika kwamba hali ya ulinzi na usalama katika mpaka huo ni ya kuridhisha.
Katika ukaguzi huo uliofanyika juzi usiku, kiongozi huyo akiambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo alitembelea vijiji vya Kibande,Nyamugali na Mnanila ambako aliambaa ambaa na ukingo wa Mto malagarasi unaotengenisha nchi za Tanzania na Burundi kuona hali halisi ya ulinzi na usalama na kuona hali ya usafirishaji wa bidhaa za magendo kupitia maeneo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari majira ya saa tisa alfajiri baada ya kukamilisha zoezi hilo, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa ulinzi shirikishi uliowekwa kuanzia ngazi za vitongoji na uelimishaji jamii kuhusu hatua za kuimarisha ulinzi maeneo ya mpakani imekuwa na mafanikio makubwa na kwamba ofisi yake itaendelea kusimamia hali hiyo kuhakikisha ulinzi na usalama wa kudumu unakuwepo wakati wote.
Sambamba na kuangalia hali ya ulinzi na usalama pia zoezi hilo lilihusisha upekuzi katika baadhi ya nyumba zilizokuwa zinahisiwa kuhifadhi wahamiaji haramu na kutembelea maeneo ya mpaka ambayo yanatuhumiwa kwa usafirishaji wa bidhaa za magendo kwenda nchini Burundi na zinazotoka huko kuingia mkoani Kigoma.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa amekuwa akifanya ukaguzi huo mara kwa mara na kwamba mafanikio ni makubwa ingawa alikiri kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya wananchi na viongozi wa vijiji katika maeneo hayo ya mpakani kushirikiana na wahalifu kutenda makosa ya uingizaji wa bidhaa zamagendo na wahamiaji haramu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Buhigwe, Anosta Nyamoga alisema kuwa zoezi la ukaguzi wa mpaka wakati wa usiku limesaidia kupunguza vitendo vya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali hasa mazao kwenda nchini Burundi bila kulipiwa ushuru.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa vitendo vya usafirishaji wa mazao na bidhaa bila kulipiwa ushuru vimekuwa vikiiokosesha mapato halmashauri yake na kwamba mkakati wa kuziba mianya ya upotevu huo wa mapato ya serikali inaendelea kufanyiwa kazi.