KIGOGO mmoja mkubwa nchini, anadaiwa kumlaza kichakani mama mjane aitwaye Irene Mbusye maarufu kama Mama Jenny, baada ya kushirikiana na benki, kununua nyumba yake ya ghorofa, iliyopo Mbezi beach jijini Dar es Salaam, kisha kuibomoa kwa lengo la kujenga nyingine, Risasi Jumamosi limeambiwa.
Katika mahojiano maalum na Risasi Jumamosi, mama huyo alisimulia jinsi ambavyo amelazimika kulala nje kwa zaidi ya miezi minne, kwa kile alichodai kuuzwa na baadaye kubomolewa kwa nyumba yake kwa kushindwa kulipa faini baada ya kuwa amelipa mkopo aliokopa kwenye benki moja ambayo jina lake linahifadhiwa kwa sasa.
“Nilianza kuishi hapa na mume wangu mwaka 1989, hii Mbezi ikiwa pori na vichaka tupu, tulijenga nyumba, mume wangu aliikuwa akijihusisha na biashara ya vifaa vya redio na meza za vioo na tukabahatika kujenga ghorofa ambayo ndiyo imebomolewa.
“Mume wangu alifariki miaka 10 iliyopita na kuniachia watoto wawili Jeniffer na Christopher, bahati nzuri nilikuwa na duka hivyo sikuwa na shida na mahitaji ya kawaida, tatizo lilikuja kwenye masomo, nikaamua kukopa kiasi fulani cha pesa benki, nikaweka hati ya nyumba na kiwanja kama dhamana, wanangu wakamaliza masomo ya sekondari, ” alisema mama huyo.
Alisema muda wa kulipa mkopo huo ulipofika, alikuwa amefanikiwa kulipa isipokuwa riba, hivyo akaomba wamvumilie kidogo hasa kwa kuwa walikuwa na hati za nyumba na kiwanja chake.
“Niliwaomba sana, lakini nikashangaa hadi mwenyekiti wa mtaa akaanza kulishabikia suala hilo, nilitarajia yeye ndiye angekuwa mtetezi wangu wa kwanza kama serikali, Machi 23, mwaka huu walikuja watu wa kampuni ya mnada na kunitaka nitoke nje na vitu vyangu, wakaniambia nyumba inapigwa mnada, nikawauliza kulikoni nyumba ipigwe mnada wakati nimeshaomba nipewe muda kidogo nimalizie penati yao, hawakunielewa ikabidi niwe nalala dukani.
“Mwanangu wa kiume alikuwa akilala kwenye gari moja lililokuwa hapa jirani, lakini mwanzoni mwa mwezi wa nne, lilikuja tingatinga na kusimama pale nje, wakijadiliana namna ya kuanza kubomoa na mwenyekiti akiwepo, wakashauriana kuwa gari lilikuwa dogo haliwezi kubomoa ghorofa, nikawa nahoji kwa nini wabomoe nyumba?
“Wakaondoka na kurudi kesho yake na kuanza kubomoa, nikakimbilia polisi na mwenyekiti akaitwa, lakini akawadanganya askari mimi nikaonekana mwomgo, lakini wale vijana waliokuwa wanabomoa walikamatwa na kulazwa ndani, baadaye waliachiwa huru na wakarudi tena kumalizia kubomoa nyumba nzima, kwa sasa nalala hapa nje kwenye hiki kichaka, duka langu lilibomolewa na vyombo vyote viliharibiwa na kubakiwa na vitu vichache, vingine vikiwa nje na kuna baadhi ya vichache nilivihifadhi kwa jirani.
“Nina zaidi ya miezi minne nalala nje, mvua na jua ni vyangu, wanangu ni wakubwa, wa kike ameolewa wa kiume alichukuliwa na rafiki zake, naomba nisaidiwe, kwa nini nyumba yangu ibomolewe? Tayari kesi ilishaenda mahakamani na nilishakutana na Lukuvi (William, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), akasema tusubiri kwa kuwa kesi iko mahakamani, lakini aliwapigia watu wa benki hiyo kama ni sahihi kubomoa nyumba ya mdaiwa.
“Ninaambiwa kuna kigogo mkubwa wa serikali, ndiye yuko nyuma ya sakata hili, eti naambiwa amenunua nyumba, yaani maelezo yanakanganya sana, naonewa kwa vile mimi ni mjane, naombeni nisaidiwe,” alisema Mama Jenny.
Risasi Jumamosi lilifika ofisini kwa mwenyekiti huyo na kukuta wasaidizi wake waliodai bosi wao amesafiri, hivyo hawawezi kutoa ufafanuzi wa jambo lolote linalomhusu kwani wao si wasemaji wa ofisi na mtaa huo.
chanzo:gpl